Fred Ngoma ni mwananchi
Klabu ya Yanga imekamilisha usajili wa kiungo mkabaji namba 6, Fred Duval Ngoma, raia wa Jamhuri ya Congo Brazzaville, akitokea klabu ya Olympique de Safi inayoshiriki Ligi Kuu ya Morocco Botola Pro.
Ngoma, mwenye umri wa miaka 28, anatajwa kuwa miongoni mwa viungo wenye uwezo mkubwa wa kucheza mbele ya safu ya ulinzi kutokana na uwezo wake wa kukaba, Mbali na nafasi yake ya kiungo mkabaji, pia ana uwezo wa kucheza kama kiungo wa kati pale inapohitajika.
Katika msimu wa 2025,26 akiwa na Olympique de Safi, Ngoma alikuwa mchezaji muhimu wa kikosi hicho, akicheza mechi nyingi za ligi na kuonyesha kiwango cha juu cha uthabiti katikati ya uwanja. Kabla ya kutua Morocco, aliwahi kuzichezea klabu mbalimbali barani Afrika na pia amewahi kuitwa katika timu ya taifa ya Congo Brazzaville.
Usajili wa Fred Ngoma unaonekana kuwa sehemu ya mkakati wa Yanga kuimarisha safu ya kiungo kuelekea msimu mpya wa mashindano ya ndani pamoja na michuano ya kimataifa.Ujio wake unatarajiwa kuongeza ushindani mkubwa katika eneo la kiungo na kuipa timu nguvu zaidi katika kulinda safu ya ulinzi na kudhibiti mchezo wa katikati.
