KIKOSI cha Simba SC kimeondoka Alfajiri ya leo kwenda Mali kwa ajili ya mchezo wake wa pili wa Kundi D Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya wenyeji, Stade Malien ya Mali Jumapili ya Novemba 30 Uwanja wa Machi 26 Jijini Bamako.
Simba SC imeondoka na kikosi cha wachezaji 21 kwa ajili ya mchezo huo wa ugenini, wakiwemo makipa wawili — Yakoub Suleiman Ali na Hussein Abel.
Simba inahitaji ushindi katika mchezo huo ili kufufua matumaini ya kwenda Robo Fainali baada ya Jumapili Simba SC kuanza vibaya hatua ya makundi ya michuano hiyo ikifungwa 1-0 na Petro de Luanda ya Angola Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam.
Bao pekee lililoizamisha Simba SC lilifungwa na kiungo Mreno, Bernardo Oliveira Dias dakika ya 78 alipofumua shuti la umbali wa Nita 20 ambalo lilimbabatiza beki raia wa Afrika Kusini, Rushine De Reuck na kubadili njia likimpoteza mwelekeo kipa namba moja Tanzania, Yakoub Suleiman Ali.
Mechi nyingine ya Kundi D Jumapili Espérance ililazimishwa sare ya bila mabao na Stade Malien ya Mali Uwanja wa Hammadi Agrebi, Tunisde Jijini Tunis nchini Tunisia.
Wakati Simba inakwenda Mali kwa mchezo wa pili wa Kundi D, Petro de Luanda wanarejea nyumbani kuwakaribisha Espérance de Tunis November 29 Uwanja wa Novemba 11 Jijini Luanda.










