Wakala wa Feitoto aikataa Yanga

Jasmine Razack, mtaalamu wa masuala ya sheria katika michezo na msimamizi wa mchezaji Feisal Salum, amekanusha Vikali Madai ya Yanga Kwamba Watalipwa endapo mchezaji huyo atauzwa, ndani au nje ya nchi.
:
Yasmin ameeleza kuwa taarifa hizo ni za kupotosha na hazina msingi wowote wa kisheria, huku akisisitiza kuwa hakuna kipengele kama hicho katika makubaliano kati ya Feisal na Azam FC.
:
“Napenda kuweka wazi kuwa hakuna mkataba unaosema Yanga watalipwa chochote kama Feisal atauzwa. Hizo ni propaganda zisizo na ukweli wowote. Tushamvumilia sana mtu akae na uvumi huu. Sasa tunalazimika kusema ili kulinda heshima ya mchezaji,” alisema Jasmine kwa msisitizo.
:
Kwa siku kadhaa sasa, mitandao ya kijamii imejaa taarifa zinazodai kuwa Yanga walijihakikishia asilimia 25 ya mauzo ya Feisal endapo atauzwa nje ya nchi, au fidia ya shilingi Bilioni Moja iwapo atauzwa ndani ya ligi ya Tanzania jambo ambalo limeibua mjadala mkubwa miongoni mwa wadau wa soka.
:
Jasmine amesema ni muhimu kwa watu kutoa taarifa sahihi badala ya kutumia jina la mchezaji kwa maslahi binafsi akitaja baadhi ya wachambuzi kutumikishwa kupotosha suala hilo.
:
“Feisal yupo Azam FC kwa mkataba halali, hana mgogoro na mtu, na hatuwezi kuruhusu jina lake litumike ovyo. Tunawaomba wahusika waache mara moja,” aliongeza.
:
Hadi sasa, Yanga SC haijatoa kauli rasmi kufafanua kuhusu madai hayo.