Jeuri ya pesa Yanga SC, Percy Tau ndani ya nyumba


Dau la kuvutia walilopata baada ya kuondoka kwa Stephane Aziz Kl Yanga, kumeifanya klabu hiyo mapema kuingia sokoni kumsaka mbaadala wake ambapo hadi sasa ina majina ya wachezaji wawili walio kwenye hatua nzuri ya kumalizana nao.

Yanga SC imemuuza Aziz KI kwenda Wydad Casablanca ya Morocco na tayari nyota huyo ameondoka akiiacha timu hiyo ikimalizia Ligi Kuu Bara na fainali ya Kombe la FA.

Katika kumpata mrithi sahihi wa Aziz KI, Yanga SC ipo kwenye mazungumzo na uongozi unaomsimamia winga wa zamani wa Al Ahly ya Misri, Percy Tau raia wa Afrika Kusini.

Tau ambaye kwa sasa anaichezea Qatar SC aliyojiunga nayo Januari mwaka huu akitokea Ahly, inaelezwa hafurahishwi na maisha ya huko inapopatikana klabu hiyo yenye makazi yake jijini Doha.

Uamuzi wa Yanga SC kuanza mazungumzo ya kumsajili Tau, ni uhitaji wao wa mchezaji ambaye atakuwa na uwezo mkubwa na kuisaidia timu kama ilivyokuwa kwa Aziz KI.