Na Prince Hoza
KITENDO cha Wekundu wa Msimhazi, Simba SC kutinga hatua ya fainali ya kombe la Shirikisho barani Afrika, sifa kemkem zinaelekezwa kwa kocha mkuu wa timu hiyo Fadlu David's raia wa Afrika Kusini.
Imepita miaka 32 Simba kuingia fainali ya michuano ya CAF, ilifanya hivyo mwaka 1993 ilipofanikiwa kuingia fainali ya kombe la CAF ambalo sasa ni Shirikisho, likiunganishwa mwaka 2004 na kombe la Washindi.
Simba ilikutana na timu ya Stella Abidjan ya Ivory Coast ambapo katika mchezo wa kwanza uliofanyika Ivory Coast timu hizo mbili zilitoshana nguvu kwa kutoka sare isiyo na mabao 0-0.
Mchezo wa pili wa fainali uliofanyika uwanja wa Taifa, sasa Uhuru jijini Dar es Salaam na Simba ilifungwa mabao 2-0 mbele ya mgeni wa heshima, Rais wa awamu ya pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Alhaj Ali Hassan Mwinyi.
Imepita miaka 32, Simba imerudia historia yake na ikifanikiwa kuingia fainali ya kombe la Shirikisho barani Afrika ambapo imekutana na timu ya RS Berkane ya Morocco, Simba imefungwa kwa jumla ya mabao 3-1 na kombe likielekea Morocco.
Mchezo wa kwanza uliofanyika uwanja wa Manispaa ya Berkane nchini Morocco na Simba ikakubali kipigo cha mabao 2-0, lakini fainali ya pili ilifanyika uwanja wa New Amaan Stadium Zanzibar Jumapili iliyopita na timu hizo kutoka sare ya kufungana bao 1-1.
Kwa jumla Simba imefungwa mabao 3-1, kitendo cha Simba kufika fainali, sifa zote anapewa kocha Fadlu, amefanya kitu kikubwa ambacho wengine awajafanya katika miaka ya karibuni, Dragan Popadic raia wa Yugoslavia (sasa haipo) na Abdallah Kibaden ni walimu pekee kuiongoza Simba kufika fainali mwaka 1993.
Historia ya klabu hiyo iliyoandikwa, inaitaja fainali ya mwaka 1993, kwani klabu hiyo haijawahi kufika hatua hityo kubwa, nafasi nyingine kufikiwa na Klabu hiyo ni mwaka 1974 ya kufika nusu fainali ya kombe la Klabu bingwa Afrika.
Wamepita makocha mbalimbali kwenye Klabu hiyo na ambao wengine wanaheshinika sana Afrika na dunia, lakini wameishia robo fainali ya Afrika na ikafikia kwamba Simba ilifahamika kama "Mwakarobo" kwa sababu inaishia robo fainali.
Wekundu hao wa Msimhazi msimu huu wameamua wafike mbali na kufanya mabadiliko makubwa ya kusajili wachezaji wapya na kocha mpya, Simba walienda Afrika Kusini na kumchukua kocha wa zamani wa Orlando Pirates, Fadlu David's na kuwa kocha wake mkuu.
Ni kweli- Fadlu tumemuona, ni kocha nzuri kwani ameweza kukibadili kikosi cha timu hiyo na kuweza kuleta ushindani na watani wake Yanga SC , misimu kadhaa iliyopita, Yanga ilikuwa mtawala wa soka la nchi.
Mbali ya kushinda ubingwa wa bara mara tatu mfululizo, ushindani ulikuwa mdogo toka kwa watani zake Simba, bila shaka msimu huu kidogo Simba inawapa mtihani Yanga.
Lakini nikirudi kwenye ukweli wa mambo, Fadlu anasaidiwa na waamuzi, au marefa, si kwenye michuano ya ndani, kwa maana Ligi Kuu bara, kombe la CRDB na hata Ngao ya Jamii, Simba inabebwa sana hata kwenye michuano ya kimataifa.
Simba hata kufika fainali, marefa wameibeba sana, ushindi wake dhidi ya Stellanboch ya Afrika Kusini haukustaili, Simba wamesaidiwa sana na waamuzi hivyo inanipa shida kumthibitisha Fadlu kama kocha mzuri kuliko wenzake waliopita Simba.
ALAMSIKI