Wawakilishi wa Tanzania katika michuano ya kombe la Shirikisho barani Afrika, Simba SC imeandika rekodi baada ya kufanikiwa kutinga fainali kufuatia sare tasa 0-0 dhidi ya Stellenbosch ya Afrika Kusini.
Kwa matokeo hayo Simba inafuzu fainali kufuatia ushindi wa 1-0 walioupata jijini Dar es Salaam katika uwanja wa Mkapa.
Simba sasa inasubiri mshindi wa jumla kati ya CS Constantine ya Algeria na RS Berkane ya Morocco ambao wanachuana usiku huu.
Mchezo wa leo uliomalizika kwa sare tasa, VAR ikikataa bao la Stellenbosch ikidai mchezaji aliyetoa assist ya bao aliotea.
Wakati huo huo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan ameipongeza timu ya Simba kwa kuingia Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kuitoa Stellenbosch jioni ya leo nchini Afrika Kusini.
“Pongezi za dhati kwa Klabu ya Simba kwa ushindi katika mchezo wa Mashindano ya Kombe la Shirikisho la Soka Afrika (CAF Confederation Cup), na kuandika historia ya kufika fainali ya mashindano haya,” amesema Rais Dk. Samia na kuongeza;
Aidha, Mheshimiwa Rais huyo wa kwanza Mwanamke Tanzania amesema Simba imeipa heshima kubwa nchi na amewatakia kila la heri katika hatua inayofuata.