Na Prince Hoza
WAAMUZI wa Tanzania Ahmed Arajiga, Kassim Mpanga, Said Hamdani na Salum Nasir wameteuliwa na FIFA kuchezesha mchezo wa kufuzu Kombe la Dunia, Botswana vs Algeria utakaochezwa Frenchtown, Botswana Machi 21, 2025.
Arajiga ni mwamuzi wa kiwango cha juu hapa nchini na ndio maana anaaminiwa na Shirikisho la soka la kimataifa duniani, FIFA na la Afrika, CAF.
Nawashangaa na nitaendelea kuwashangaa baadhi ya Watanzania hasa wapenzi wa soka kumkataa mwamuzi huyo wakidai anachezesha vibaya kwenye baadhi ya mechi za Ligi Kuu bara.
Mimi binafsi sikubaliani nao, Arajiga ni mwamuzi bora na ataendelea kuwa bora, uzuri wa Arajiga anapenda haki, anachezesha bila kuuma na muumini wa haki.
Amekuwa akitumika mara kwa mara kwenye mechi za kimataifa za FIFA au CAF na kwenye mechi kubwa za hapa nchini amekuwa akisimama zote, mwamuzi huyo amesimama kwenye derby ya Simba SC na Azam FC.
Wapo baadhi ya watu wanampinga mwamuzi huyo wakidai si mzuri kwa maamuzi, wale wanaomkataa Arajiga ni miongoni mwa watu wanapenda dhuluma.
Kwasasa malalamiko ni mengi kwenye Ligi Kuu bara, wanaolalamika wanadai waamuzi ni tatizo, zipo baadhi ya timu zinapendelewa waziwazi na waamuzi na hakuna onyo au adhabu kwa wanaokosea.
Mifano ya uharibifu wa Sheria 17 za FIFA zimefanywa sana kwenye baadhi ya mechi ila naweza kutaja mechi moja au mbili zitakazozigusia, mwamuzi aliyechezesha mechi kati ya Namungo FC na Simba SC aliboronga sana.
Katika maamuzi yake alitoa penalti tatu kwa Simba SC ambapo mbili waliziweka kimiani na moja walipoteza, lakini mwamuzi huyo alimpa kadi nyekundu mchezaji wa Namungo FC, Derick Mukombozi bila kuonekana kosa lake.
Mwamuzi huyo aliwatoa michezoni Namungo na kusababidha wapoteze mchezo, baadaye Kamati ya Masaa 72 iliketi na ikabaini kwamba mwamuzi huyo alimuonea Mukombozi na ikaamua kuifuta kadi hiyo.
Mechi nyingine ambayo Mashujaa FC ilicheza na Yanga SC, katika mchezo huo Yanga ilishinda mabao 5-0, lakini mwamuzi wa mchezo huo aliwanyima penalti ya wazi Mashujaa FC.
Inawezekana waamuzi wa ligi yetu hawajui vema kuchezesha isipokuwa wanapangiwa mechi Ili mradi, na ndio maana sasa Shirikisho la soka nchini, TFF imeanza kuwapiga msasa waamuzi hao.
Mechi nyingi wanazocheza Simba na Yanga, waamuzi wanaboronga, Simba na Yanga zinabebwa sana, sitaki kuweka wazi kila kitu ila nawaambia waamuzi wengine wajifunze kwa Arajiga ambaye amekuwa makini kazini.
Shida ya baadhi ya waamuzi (SIO Arajiga) hawako makini kazini kwao, anachosimamia yeye mchezaji akianguka hata kwa bahati mbaya yeye ananyoosha kati, iwe penalti au faulo.
Inachekesha sana mchezo kati ya Namungo na Dodoma Jiji, mchezaji wa Namungo kaunawa yeye kwenye boxi ya 18 ya Dodoma Jiji, lakini mwamuzi anawapa penalti Namungo jambo ambalo si haki.
Arajiga ana mchezo wa namna hiyo, anasimamia haki na wala hataki upuuzi, wachezaji wetu wanakatabia cha kujiangusha kwenye 18 ya pinzani, endapo mwamuzi hayuko makini anatoa penalti na ndio maana waamuzi hupata malalamiko kwani si penalti halali
Kuna la kujifunza kwa Arajiga, kila ninaposoma post za TFF kuhusu waamuzi wanaokwenda kuchezesha mechi nje ya nchi, Arajiga na Frank Komba nawaona mara kwa mara, Arajiga ni bonge la mwamuzi hivyo wengine wanapaswa kuiga mazuri yake.
ALAMSIKI