IVO Philip Mapunda ni miongoni mwa makipa bora katika historia ya soka la Tanzania, akijulikana kwa umahiri wake wa kupangua penalti na kudhibiti mashambulizi hatari. Alizaliwa Novemba 14, 1979, katika kijiji cha Kisa Ushirika, Safari yake ya soka ilianzia katika viunga vya Kisa Ushirika, Tukuyu Mbeya, mji wenye mandhari nzuri ya milima, mashamba ya chai, na hali ya hewa ya baridi, kisha kusambaa hadi nje ya mipaka ya Tanzania, akitamba katika vilabu kadhaa
Akiwa mdogo, alisomea Kisa na Nyololo, kisha akasoma Mechanics katika Shule ya Ufundi Ifunda. Ingawa alipata nafasi ya kuendelea na masomo ya ufundi, aliamua kufuata ndoto yake ya soka. Alianza kucheza Mpuguso Stars kisha Tukuyu Stars, ambapo aling’arisha kipaji chake kabla ya kusajiliwa na Tanzania Prisons.
Akiwa Prisons, aliingia rasmi Jeshi la Magereza na kuwa Koplo, lakini alipotaka kuihama timu, alikumbwa na matatizo hadi kufungwa jela. Baada ya kutoka, alijiunga na Moro United (2005), kisha akasajiliwa na Yanga SC (2006-2009). Alicheza Ethiopia na Saint-George kwa msimu mmoja kabla ya kurejea Tanzania na kuichezea African Lyon.
Mwaka 2012, alihamia Kenya na kucheza Bandari FC, kisha Gor Mahia (2013), ambako aliendelea kung'ara. Baada ya muda Kenya, alirudi Tanzania na kucheza Simba SC na Azam FC kabla ya kustaafu soka na kuingia katika ukocha.
Katika timu ya taifa, Ivo aliichezea Taifa Stars tangu 2006 na kushiriki mechi zaidi ya 17.
Umahiri wake ulichanganywa na ujasiri wake akiwa langoni, huku taulo lake likihusishwa na imani za kishirikina, ingawa mafanikio yake yalitokana na bidii na mazoezi makali.
Safari ya Ivo Mapunda ni ushuhuda wa kujituma na nidhamu, kutoka mitaa ya Tukuyu hadi soka la kimataifa. Sasa akiwa kocha, anaendelea kuchangia maendeleo ya soka la Tanzania.