SIMBA KUWAACHA BALEKE NI PHIRI NI KUJIMALIZS AU KUJIJENGA UPYA?
Na Prince Hoza
KLABU ya Simba SC maarufu Wekundu wa Msimbazi imewaacha washambuliaji wake hatari Moses Phiri raia wa Zambia na Jean Baleke raia wa DR Congo, Simba imeamua kuwaacha washambuliaji hao baada ya kutoridhishwa na viwango vyao.
Mbali na kuwaacha washambuliaji hao, pia imewaacha na wachezaji wengine wazawa, klabu hiyo imeamua kufanya mabadiliko kwa kuwasajili wachezaji wapya wakiwemo washambuliaji na wa maeneo mengine.
Baada ya kutangaza kuwaacha washambuliaji hao, zimetoka lawama kutoka kwa baadhi ya mashabiki wake na wadau wa soka wakishangaa
kuwaacha Baleke na Phiri ingawa takwimu ziliwabeba.
Nikianza kwa Phiri, takwimu zilimbeba mshambuliaji huyo aliyejiunga na Simba msimu uliopita akitokea Zanaco ya Zambia.
Mshambuliaji huyo alifanikiwa kufunga mabao 10 kwenye Ligi Kuu bara akiongoza kwa mabao kwenye timu yake na pia akishika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu bara akiwa nyuma ya Fiston Mayele aliyekuwa anaichezea Yanga SC.
Hata hivyo Phiri aliumia katika ligi ikiwa inaendelea na kuumia kwake kulimuathiri katika ndoto zake za kuchukua kiatu cha dhahabu.
Mwishoni mwa msimu Said Ntibanzokiza "Saido", John Bocco na Jean Baleke waliweza kuonyesha uwezo wao wa kufunga na kumpa changamoto Phiri.
Pia Mzambia huyo alikuwa msaada mkubwa Simba kwenye michuano ya Ligi ya mabingwa Afrika akiiwezesha Simba kutinga hatua ya makundi huku yeye akiwa mmoja kati ya wafungaji wa timu.
Hata msimu huu kwenye mechi za Ligi Kuu bara aliweza kupachika mabao matatu ingawa akucheza mechi nyingi.
Kwa kifupi Simba imemuacha Phiri akiwa bado ana uwezo mkubwa wa kupachika mabao ingawa kwa mujibu wa kocha Abdelhak Benchikha anadai kwamba Phiri si lolote na timu yake inahitaji mshambuliaji hatari.
Kwa upande wa Baleke, ambaye naye alijiunga na Simba kwa mkopo akitokea TP Mazembe ya DR Congo, alikuja kwenye dirisha dogo na aliweza kufunga mabao 9, moto wake wa mabao uliwatisha wengi na ikabidi apewe nafasi zaidi na msimu huu alikuwa tegemeo la timu.
Mpaka Ligi Kuu bara inasimama kupisha kombe la Mapinduzi, Baleke alishapachika magoli 8 na assist moja katika mechi 9 alizocheza ni sawa na kuhusika na magoli kwenye mechi zote.
Msimu uliopita Baleke alikuwa msaada mkubwa kwenye Ligi ya mabingwa Afrika katika hatua ya makundi, ambapo atakumbukwa kwenye mchezo wa Raja Casablanca na Wydad ambapo aliweza kupachika mabao.
Sio siri Benchikha amependekeza Baleke na mwenzake Phiri waachwe akiamini kwamba hawana viwango vya kuipigania Simba.
Binafsi mimi naona ni kama Simba inajimaliza yenyewe, lakini kwa upande wangu wa pili ni kama Simba inaenda kujijenga upya.
Kabla ya ujio wa Benchikha, Simba ilikuwa inanolewa na Mbrazil Robert Oliviera "Robertinho" lakini kilio kikubwa cha Wanasimba ni kukosa matokeo mazuri na washambuliaji walionekana tatizo, ngoja tuone na tusubiri.
ALAMSIKI