Kaseja mchezaji bora Januari
Na Mrisho Hassan. Dar es Salaam
Golikipa wa timu ya Kagera Sugar, Juma Kaseja amechaguliwa kuwa mchezaji bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara wa mwezi Januari kwa msimu wa 2016/2017.
Kaseja aliwashinda wachezaji Mbaraka Yusuph pia wa Kagera Sugar na Jamal Mtengeta wa Toto Africans.
Katika mechi tatu ambazo timu ya Kagera ilicheza kwa mwezi huo, Kaseja ambaye alicheza kwa dakika zote 270 alikuwa kiongozi na mhimili wa timu na aliisaidia timu yake kupata ushindi katiks michezo yote ambapo ilikusanya jumla ya pointi 9 zilizoifanya timu hiyo kupanda nafasi mbili katika msimamo wa ligi kwa mwezi huo wa Januari kutoka nafasi ya 5 hadi ya 3.
Katika michezo hiyo mitatu Kagera Sugar ilifunga mabao sita na Kaseja alifungwa bao moja tu na alionyesha nidhamu ya hali ya juu ikiwemo kutopata onyo lolote (Kadi).
Kwa kushinda tuzo hiyo Kaseja atazawadiwa kitita cha sh 1,000,000 (Milioni moja) kutoka kwa wadhamini wa ligi hiyo Kampuni ya Vodacom Tanzania