MAKALA: SIMBA ITAJUTIA MAAMUZI YAKE
Na Prince Hoza
Simba SC inaelekea kubaya, nina maana viongozi wake wanakurupuka kwa kutoa maamuzi yasiyo na tija kwa mashabiki wake, Simba kwa sasa inakamata nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara.
Timu hiyo ilikuwa ikiongoza ligi hiyo kwa kipindi kirefu lakini jana iliondolewa rasmi kileleni hasa baada ya jana Yanga SC kushinda mabao 2-0 dhidi ya Mwadui FC ya Shinyanga katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam mchezo wa Ligi Kuu Bara.
Yanga waaongoza kwakuwa na pointi 46 wakati Simba iliyofungwa bao 1-0 na Azam juzi Jumamosi katika uwanja huo huo wa Taifa ina pointi 45, tatizo linaloonekana kuiathili Simba ni kukosekana kwa muunganiko wa pamoja wa wachezaji wake.
Benchi la ufundi linaloongozwa na Mcameroon Joseph Omog libaonekana kushindwa kufanya kazi yake ipasavyo, lakini mimi wala simlaumu hata kidogo Omog kwani karibu wachezaji wote walioko Simba hakuhusika katika usajili wao.
Wachezaji wa Simba walisajiliwa kwa matakwa ya viongozi na wanachama wao na ushabiki ulihusika zaidi, Omog alisajiliwa wachezaji na akapewa akaambiwa ni wazuri na ubingwa ni ajenda yao msimu huu.
Kamati ya usajili ya Klabu hiyo inayoongozwa na mwenyekiti wake Kapteni mstaafu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Zacharia Hanspope akawatangazia Wanasimba kuwa straika Hamisi Kiiza raia wa Uganda hafai mnafiki hasa baada ya msimu uliopita kuanzisha mgomo baridi wa wachezaji wa kigeni.
Kiiza aliwaongoza wachezaji wenzake wa kigeni kugomea ili walipwe pesa zao za mishahara, mgomo huo uliungwa mkono na Jjuuko Murushid, Brian Majwega, Poul Kiongera, Vincent Angban na Justuce Majabvi, na baadaye nyota hao wakaachwa na wawili tu ndio walionusurika ambao ni Jjuuko na Angban aliyeachwa msimu huu.
Kiiza ambaye aliibuka mfungaji bora kwenye kikosi cha Simba akifanikiwa kufunga mabao 19 akishika nafasi ya pili nyuma ya Amissi Tambwe aliyeibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Tambwe alifunga magoli 21 na kutwaa kiatu cha dhahabu.
Kilichonishangaza kwa viongozi wa Simba kwamba wameamua kumuacha Kiiza kwa madai eti ni mtovu wa nidhamu kwa sababu amewadai oesa zake za mshahara, kwani kudai haki yako ni kosa? Viongozi wa Simba wametudanganya kwa kusema Kiiza hafai na wamsajili straika Laudit Mavugo kutoka Burundi.
Mpaka sasa Mavugo amefunga magoli matano tu, hii ni mara ya pilj kwa Simba kuachana na wafungaji wake wazuri, iliwahi kumtema Amissi Tambwe aliyeibuka mfungaji bora kwa kufunga magoli 19 na msimu uliofuata akatua zake Yanga ambapo yupo hadi sasa.
Kwakweli Simba watajutia sana maamuzi yao ambayo yanawagharimu, nina imani kama angekuwepo Kiiza huenda tungeshuhudia Simba ya mwendokasi ambayo ingekuwa suluhisho kwa mashabiki wake.
Ila bado sijawakatia tamaa wanaweza kutwaa ubingwa kama watayafanyia kazi mapungufu yaliyopo, tatizo ambalo naliona pale ni kukosekana kwa mshambuljaji namba moja ambaye yeye kazi yake ni kucheka na nyavu, Mavugo na wengine waliopo Simba ni washambuliaji namba mbilj kwa mfano Ibrahim Ajibu, Mohamed Ibrahim na Juma Luizio