ERICK MAJALIWA: Alisababisha mgogoro mkubwa wa kiuongozi Simba, inadaiwa ni mtoto wa waziri mkuu
HISTORIA imeandikwa katika soka la Tanzania hasa baada ya Rais wa
jamhuri ya muungano Mhe John Pombe Magufuli kumteua mbunge wa
Ruangwa mkoani Lindi Majaliwa Kasimu Majaliwa kuwa Waziri mkuu wa
11 wa Tanzania.
Uteuzi huo ulipokelewa kwa hisia tofauti toka kwa Watanzania, wapo
walioshangazwa na uteuzi huo ambao waliamini huenda lingetangazwa
jina kubwa lililozoeleka masikio mwao, na wengine walishangaa tu
kuona Naibu waziri TAMISEMI wa serikali ya Awamu ya nne anakuwa
waziri mkuu serikali ya Awamu ya tano.
Pia uteuzi huo uliwashangaza wanamichezo, hawakutarajia kabisa
kusikia mwanamichezo mwenzao anateuliwa na Rais kuwa waziri mkuu,
mhe Majaliwa ni kocha wa soka mwenye leseni B inayotambulika na
CAF, Majaliwa pia ni kocha wa timu ya Bunge FC huku pia akikinoa
kikosi cha Wabunge wanaoshabikia Simba SC.
Kwa mashabiki wa Simba walilipuka furaha kwani Mhe Majaliwa ni
Simba mwenzao tena damu, lakini kikubwa zaidi Mhe Majaliwa ni baba
wa kiungo wa zamani wa Simba, Erick Majaliwa.
Wakati anateuliwa tu rais Magufuli, kwenye mitandao ya kijamii
ziliibuka taarifa zake kuwa ni baba wa kumzaa Erick Majaliwa, Erick
aliwahi kuichezea imba mwanzoni mwa miaka ya 2000 ingawa hakudumu
sana , mchezaji huyo alisajiliwa na Simba baada ya kumuona akicheza
vizuri kwenye timu ya shule ya sekondari ya Makongo iliyokuwa
ikisimamiwa na Kanali mstaafu Idd Kipingu, Makongo ilisifika kwa
kutoa wachezaji mbalimbali hapa nchini.
Erick alikuwa mchezaji mzuri mwenye nidhamu na uwezo wa kucheza
nafasi tofauti, nyota huyo wa zamani wa Simba hakuwahi kutamba sana
lakini aliweza kujizolea sifa kemkem, Erick aliwavutia wengi
kutokana na kiwango chake licha ya kukutana na changamoto ya namba.
Wakati huo Simba ilikuwa na mastaa lukuki ambao walisababisha nyota
huyo kushindwa kuunguruma na kuishia benchi, Majaliwa asingeweza
kupata namba mbele ya Haruna Moshi 'Boban' hivyo uongozi wa Simba
uliamua kumtoa bure kwa timu ya Al Shaab Hadramaut ya Yemen.
Majaliwa aliungana na kocha wake Jamhuri Kihwelu 'Julio' ambaye
naye aliwahi kuichezea Simba na baadaye kuifundisha akiwa kama
kocha msaidizi, inadaiwa aliyekuwa katibu mkuu wa Simba Mwina Seif
Kaduguda ndiye aliyemwidhinishia kujiunga bure na timu hiyo ya
Yemen.
Waziri mkuu Mhe Kasimu Majaliwa akikabidhi bendera kwa timu ya vijana
Timu hiyo ya Yemen iliyokuwa ikishiriki ligi kuu ilikusanya
wachezaji lukuki kutoka Tanzania ambao wote walipatiwa vibali vya
uhamisho, wachezaji wengine walioungana na Majaliwa ni Monja
Liseki, John Njama na Omari Changa (sasa marehemu).
Baadaye viongozi wa Simba waliingia katika mzozo mkubwa kufuatia
mchezaji huyo kuruhusiwa bure bila klabu kuingiza kiasi chochote,
Kaduguda na mwenyekiti wa Simba Hassan Dalali walishutumiana
waziwazi, huenda Erick Majaliwa kwa sasa anaangukia kwenye neema
nyingine baada ya ile ya kuichezea Simba kama ni kweli mtoto wa
waziri mkuu