NGOMA, KIIZA WATISHA KWA MABAO LIGI KUU BARA 2015/16

Yanga ilishinda 2-0 katika mechi yake ya ufunguzi wa msimu Jumapili iliyopita dhidi ya Coastal Union kupitia mabao ya Mzimbabwe, Donald Ngoma, na mzawa Simon Msuva, wakati katika mechi yao ya pili mabingwa hao walishinda 3-0 dhidi ya Tanzania Prisons kupitia magoli ya beki wa Rwanda, Mbuyu Twite, Mrundi Amisi Tambwe na Mzimbabwe, Donald Ngoma.

Mahasimu wao, Simba, kufikia sasa wamefunga jumla ya magoli matatu, mawili yakifungwa na Mganda Hamis Kiiza na moja Mzimbabwe, Justice Majabvi. Wekundu wa Msimbazi walishinda 1-0 dhidi ya African Sports katika mechi ya ufunguzi kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga kabla ya kuilaza Mgambo Shooting 2-0 juzi kwenye uwanja huohuo.

Washindi wa pili wa msimu uliopita, Azam FC, kufikia sasa baada ya mechi mbili za ligi hiyo ya juu zaidi nchini, wamefunga jumla ya magoli manne, mawili ya nyota wa kigeni Muivory Coast, Kipre Tchetche na Mkenya, Allan Wanga huku mengi mawili yakifungwa na Farid Mussa na Frank Domayo. Azam ilishinda 2-1 dhidi ya Prisons kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam kabla ya juzi kuilaza Stand United 2-0 kwenye Uwanja wa Kambarage, Shinyanga.

Mabao 17 ya juzi ni ongezeko la mabao sita zaidi ya yaliyofungwa katika raundi ya kwanza msimu huu na mawili zaidi ya ilivyokuwa raundi ya pili msimu uliopita.


Mshambuliaji Donald Ngoma wa Yanga, ana mabao mawili kama mwenzake Hamisi Kiiza wa Simba

Katika jumla ya mabao 28 yaliyofungwa katika raundi mbili za kwanza msimu huu, mabao 9 yamefungwa na wageni, sawa na asilimia 32 ya mabao yote. Ligi Kuu ya Bara msimu huu ina jumla ya wachezaji 29 wa kigeni. Simba, Yanga na Azam zinao nyota wa kigeni 7 kila moja, Coastal Union wanne, Stand United (2), Mbeya City (1) na African Sports mmoja. 

Mabao 11 ya raundi ya pili juzi yalifungwa na timu mwenyeji huku wachezaji Miraji Athuman (Toto), Donald Ngoma (Yanga), Hamis Kiiza (Simba) na Atupele Green (Ndanda) wakifunga bao moja na kufikisha mabao mawili kila mmoja msimu huu baada ya kutupia pia bao moja-moja katika mechi za raundi ya kwanza Jumamosi na Jumapili.

Mabao mawili yalifungwa kwa penalti na Ngoma na Themi Felix wa Mbeya City wakati beki wa Prisons James Josephat aliweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza kutolewa kwa kadi nyekundu msimu huu baada ya kumkwatua winga, Simon Msuva na kusababisha penalti.  Yanga imecheza mechi mbili bila wachezaji wake kuonyeshwa kadi hata moja ya njano.  Kiungo Nizar Khalfan wa Mwadui FC ndiye ameweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza kukosa penalti baada ya kushindwa kufunga kwa ‘tuta’ katika mechi yao ya kwanza waliyolala 1-0 dhidi ya Toto Africans jijini Mwanza Jumamosi.

Matokeo ya mechi za juzi yalikuwa Yanga 3-0 Prisons, Majimaji 1-0 Kagera, Mbeya City 3-0 JKT Ruvu, Ndanda 1-0 Coastal, Mwadui 2-0 A/Sports, Stand 0-2 Azam, Toto 1-2 Mtibwa, na Mgambo 0-2 Simba.
Katika raundi ya pili ya VPL msimu uliopita (timu zilikuwa 14) mabao 15 yalifungwa (sita yalifungwa na timu zilizocheza ugenini, sawa na msimu huu).

Matokeo ya raundi hiyo msimu uliopita yalikuwa Simba 1-1 Police Moro, Mtibwa 3-1 Ndanda, Azam 2-0 Ruvu Shooting, Mbeya City 1-0 Coastal, Mgambo 0-1 Stand, JKT Ruvu 0-2 Kagera, na Yanga 2-1 Prisons.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA