NGASSA AWAFUNIKA MBWANA SAMATTA, ULIMWENGU

MSHAMBULIAJI wa Yanga SC ya Dar es Salaam, Mrisho Khalfan Ngassa anaweza akawa mfungaji bora wa Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu, michuano hiyo ikiwa imefikia hatua ya Nusu Fainali.

Taarifa ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) imesema kwamba, Ngassa hadi sasa anaongoza kwa mabao yake sita baada ya hatua ya awali na ya makundi ya michuano hiyo.Ngassa alicheza mechi nne tu za Raundi mbili za awali za michuano hiyo, dhidi ya Komorozine ya Comoro nyumbani na ugenini, akifunga mabao matatu kila mechi.

Baada ya hapo akacheza vizuri katika mechi zote mbili dhidi ya Al Ahly ya Misri, Yanga SC ikitolewa kwa penalti baada ya sare ya jumla ya 1-1, kila timu ikishinda 1-0 nyumbani kwake.

Lakini tangu hapo, wachezaji waliofanikiwa kumkaribia Ngassa kwa mabao msimu huu kwenye michuano hiyo ni watano, Haithem Jouini wa Esperance ya Tunisia, Edward Takarinda Sadomba wa Al Ahli Benghazi ya Libya, Iajour Mouhssine wa Raja Club Athletic ya Morocco na Knowledge Musona wa Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini, ambao kila mmoja amefunga mabao matano pia, lakini timu zao zimekwishatolewa.Mubele Ndombe wa AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), ndiye pekee mwenye mabao matano na timu yake imekwenda Nusu Fainali.


Wenye mabao manne kila mmoja ni Benyoussef Fakhreddine wa Sfaxien ya Tunisia, El Hedi Belameiri wa E. S. Setif ya Algeria, wakati Abdelrahman Ramadan Fetori wa Benghazi ana matatu, sawa na Abdoulaye Ssissoko wa Stade Malien ya Mali, Ahmed Akaichi wa Esperance, Akram Djahnit wa E. S. Setif, Cesair Gandze wa AC Leopards ya Kongo, Driss Mhirsi wa Esperance, Etekiama Agiti Taddy wa AS Vita ya DRC, Kingston Nkhatha wa Kaizer Chiefs na Lamine Diawara wa Stade Malien.
Kwa kuwa michuano hiyo imefikia kwenye hatua ngumu ya Nusu Fainali- ambayo si rahisi timu kufungana mabao mengi,

Ngassa ana nafasi kubwa ya kutawazwa kuwa mfungaji bora msimu huu, licha ya kwamba Yanga SC haikufika hata hatua ya makundi.

 TP Mazembe itakutana na ES Setif ya Algeria katika Nusu Fainali, wakati AS Vita itakutana na CS Sfaxien ya Tunisia, mechi za kwanza zikichezwa kati ya Septemba 19 na 21 na marudiano kati ya Septemba 26 na 28.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA