WAMBURA, KABURU KUENGULIWA UCHAGUZI MKUU SIMBA

Michael Wambura na Geofrey Nyange ‘Kaburu’ pamoja na wagombea  wa ujumbe wa kamati ya utendaji ya Simba wamewekewa pingamizi la kuwania uongozi.

Mwanachama Swaleh Madjapa kadi namba 00574, Mwinyi Dossy kadi namba 564 pamoja na kocha wa zamani wa timu hiyo, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ ndio waliojitokeza jana kuweka pingamizi kwa wagombea hao.


Mbali na Wambura na Kaburu,  wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya Simba, Swedi Nkwabi, Said Pamba, Ibrahimu ‘Maestro’, Joseph Itang’are ‘Kinesi’ na Daniel Manembe wamewekewa pingamizi na wanachama watatu tofauti kwa madai ya kukiuka katiba ya Simba.

Madjapa alimwekea pingamizi  Wambura akidai wakati akichukua fomu alifanya kampeni kinyume na taratibu na kwamba ana vielelezo vyote vinavyothibitisha kuwa Wambura alifanya kampeni kabla ya muda wake.

Wambura aliwahi kuwa mwenyekiti wa klabu hiyo, lakini akasimamishwa na uongozi baada ya kufungua kesi mahakamani kupinga kuenguliwa kwenye uchaguzi mwaka 2008, kitendo ambacho ni uvunjaji wa katiba.

Pia aliwawekea pingamizi wagombea wote ambao ni wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya Simba inayomaliza muda wake kwa kile alichoeleza kuwa kwa kipindi cha miaka minne walichokaa madarakani hakuna walichofanya cha maana kinachofanya waombe tena kupewa miaka mingine minne ili wamalizie, zaidi ya vurugu.

Naye Kihwelo, anayegombea nafasi ya makamu wa rais, aliwekea pingamizi Kamati ya Utendaji kwa kile alichodai walikiuka katiba kwa kuendesha vikao visivyo halali na kuupindua uongozi wa  Ismail Aden Rage na pia walikiuka katiba ya klabu hiyo kwa kutojaza nafasi ya makamu mwenyekiti iliyoachwa na Geofrey Nyange ‘Kaburu’ ndani ya siku 90.

Pia, wajumbe hao wa kamati ya utendaji inayomaliza muda wake waliwekewa pingamizi na Mwinyi Dossy kadi namba 564.

Kaburu aliwekewa pingamizi na mchezaji wa zamani wa klabu hiyo, Athurh Mwambeta (kadi namba 01005) ambaye pia amewekewa na Swedi Nkwabi. Mwambeta amedai Kaburu akiwa makamu mwenyekiti alikiuka katiba ya Simba ibara ya 33 (5) na 28 (1b) kwa kushindwa kuwasilisha ripoti ya mapato na matumizi ya fedha katika mkutano mkuu mwaka 2010 hadi mwaka 2013 alipojiuzulu.

Pia, alidai kuwa kwa mujibu wa katiba ya Simba kiongozi anayejiuzulu haruhusiwi kugombea tena uongozi ndani ya klabu hiyo kwa vipindi vitatu na kudai kuwa Kaburu hajafikisha vipindi vitatu toka ajiuzulu.

Kwa upande wa pingamizi la Nkwabi, Mwambeta alidai kuwa alikiuka katiba wakati wa uongozi wao kwa kuendesha mapinduzi ya kumpindua Rage. Swedi pia aliwekewa pingamizi na Lucas Mbapila kwa madai ya kukiuka kanuni za uchaguzi.

Chano Almas aliwekewa pingamizi Dossy na Madjapa kwa madai ya kukiuka katiba.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA