SIMBA KIMENUKA, YAFUMULIWA TENA NA COASTAL UNION

Kikosi cha Coastal Union kilichofanyiwa mabadiliko kikiwaacha nje nyota wa zamani wa Simba akiwamo beki Juma Nyosso na kiungo Haruna Moshi 'Boban', jana kiliwashangaza Wekundu wa Msimbazi kwa kipigo kingine kisichotarajiwa cha 1-0 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, huku Azam FC ikibaki kileleni kufuatia ushindi wa 1-0 dhidi ya JKT Oljoro.

Kilikuwa ni kipigo cha nne kwa Simba msimu huu kilichowaacha Wekundu hao katika nafasi ya nne ya msimamo wakiwa na pointi 36, wakati Azam walijiimarisha kileleni kwa kufikisha pointi 47, nne juu ya Yanga iliyo katika nafasi ya pili. Yanga imecheza mechi moja pungufu.

Azam walipata goli lao la pekee kupitia kwa John Bocco 'Adebayor' katika dakika ya 71 kwenye Uwanja wa Azam Complex, ambako timu hiyo ambayo haijapoteza mchezo hata mmoja ilionekana kama ingedondosha pointi mbili baada ya kipindi cha kwanza kumalizika matokeo yakiwa 0-0.


Kwenye Uwanja wa Taifa, Coastal walifunga goli lao katika dakika ya 44 kupitia kwa Hamad Juma aliyetumia vyema makosa ya beki wa Simba, Omary Salum, ambaye alimruhusu akauwahi mpira na kupiga shuti lililotinga wavuni.

Mpira ulianza kwa utulivu lakini katika dakika ya 8 beki wa Coastal Abdi Banda aliokoa kishujaa shuti la mshambuliaji Mrundi Amisi Tambwe lililokuwa linaelekea katika lango lao.

Katika dakika hizo za kwanza ambazo Simba walicheza vizuri, Coastal walikuwa makini kuhakikisha hawaruhusu goli la mapema. Katika dakika ya 17, Mbwana Hamis aliokoa krosi ya winga wa Simba, Ramadhani Singano 'Messi' na kuikosesha Simba nafasi ya kufunga na katika dakika ya 23 winga wa Simba, Haruna Chanongo alipiga pembeni na kupoteza pasi nzuri ya Omary Salum.

Wageni walicharuka kwa shambulizi katika dakika ya 23 lakini kipa wa Simba, Ivo Mapunda aliwahi kudaka mpira wa kichwa uliopigwa na Ally Nassor kutokea ndani ya boksi na kuikosesha Coastal nafasi ya kufunga.

Simba walikaribia kufunga katika dakika ya 73 lakini shuti la Jonas Mkude liligonga nguzo ya lango na kurejea uwanjani.

Vikosi vilikuwa; Simba: Ivo Mapunda, Haruna Shamte/ Christopher Edward (dk.62), Issa Rashid 'Baba Ubaya', Joseph Owino, Donald Musoti, Henry Joseph, Omari Salum/ William Lucian (dk.46), Jonas Mkude, Haruna Chanongo, Amisi Tambwe na Ramadhani Singano 'Messi'.

Kocha wa Coastal Union, Yusuf Chipo alielezea furaha yake kwa ushindi huo dhidi ya timu kubwa huku akisema ulichangiwa na mabadiliko ya kikosi aliyoyafanya dhidi ya kile kilichopigwa 4-0 dhidi ya Azam FC katika mechi yao iliyopita.

Alisema Simba ilicheza vyema katika dakika za kwanza lakini walipowafunga goli walichanganyikiwa na kushindwa kurejea mchezoni.

Chipo, ambaye ushindi uliifanya timu yake ifikishe pointi 29 na kukaa katika nafasi ya saba, alisema anataka kumaliza katika nafasi bora zaidi msimu huu.
Katika mechi ya mzunguko wa kwanza baina ya Simba na Coastal kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga timu hizo zilitoka 0-0.

Katika kuonyesha fadhaa, winga Singano alidaiwa kupiga teke kioo cha mlango wa kuingilia katika chumba cha kuvalia cha Simba na kukivunja.

Coastal Union: Fikirini Selemani, Hamadi Juma/ Ayoub Masoud (dk.60), Abdi Banda, Yusuf Chuma, Mbwana Hamis, Razack Khalfan, Ally Nassor/ Mohammed Mtindi (dk.35), Behewa Sembwana, Seleimani Kassim 'Selembe'/ Marcus Ndeheli (dk.75), Daniel Lyanga na Kenneth Masumbuko.

Katika matokeo mengine ya jana, Ruvu Shooting iliifunga Ashanti 2-0 kupitia magoli mawili ya Elias Maguri katika dakika ya 6 na 63, huku Mgambo ikitoka sare ya 1-1 dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Mkwakwani Tanga.


Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA