LOGARUSIC AULA SIMBA, AONGEZEWA MWAKA MMOJA ZAIDI

Licha ya timu ya Simba kusuasua kwenye mechi za Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara, uongozi wa klabu hiyo ya jijini Dar es Salaam unatarajia kumpa mkataba mpya wa mwaka mmoja kocha mkuu wa timu hiyo, Mcroatia Zdravko Logarusic, imefahamika.

Logarusic aliyetua nchini Desemba mwaka jana, alipewa mkataba wa miezi sita kuifundisha Simba huku akilipwa mshahara wa Dola za Marekani 3,000.

Kwa mujibu wa habari zilizopatikana jijini Dar es Salaam kutoka chanzo chetu kilichopo ndani ya klabu hiyo, zinaeleza kuwa uongozi wa klabu hiyo umeridhishwa na kiwango kilichoonyeshwa na kocha huyo wa zamani wa Gor Mahia ya Kenya.


Chanzo hicho kiliongeza kwamba, uongozi utampa mkataba mpya mara baada ya ligi kumalizika na itampa ruhusa fupi ya kurejea kwao kusalimia familia na kutakiwa kuwahi kurudi nchini kuendelea na zoezi la usajili wa wachezaji.

"Ana nafasi kubwa ya kupewa mkataba mpya, ila itakuwa ni baada ya msimu huu (2013/2014) kumalizika, ingawa kama binadamu ana mapungufu yake," alisema mmoja wa viongozi wajuu wa Simba.

Habari zaidi kutoka Simba zinaeleza kuwa Mkurugenzi wa Ufundi wa klabu hiyo, Moses Basena, anatarajiwa kuelekea Uganda kwa lengo la  kusaka wachezaji wenye uwezo ili waweze kusajiliwa katika msimu ujao wa ligi.

Katibu Mkuu wa Simba, Ezekiel Kamwaga, aliliambia gazeti hili kuwa ni kweli uongozi umeshaanza kumjadili kocha huyo lakini bado maamuzi rasmi hayajatolewa.

Kamwaga alisema Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo itapitisha maamuzi ya kumpa mkataba mpya Logarusic baada ya kupokea taarifa kutoka kwenye Kamati ya Ufundi.

Alieleza kuwa mkataba wa sasa wa Logarusic unatarajiwa kumalizika Mei 31, mwaka huu.

Logarusic na Kocha Msaidizi, Selemani Matola, walikabidhiwa mikoba ya kuiongoza Simba baada ya Abdallah Kibaden (King) na msaidizi, Jamhuri Kihwelu (Julio) kutimuliwa.

Simba ina pointi 36 na iko katika nafasi ya nne katika msimamo wa ligi hiyo inayoshirikisha timu 14 kutoka mikoa mbalimbali hapa nchini ambayo itamalizika Aprili 19, mwaka huu.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA