OKWI KUONGOZA MAUAJI YANGA LEO

Yanga leo inashuka kwenye Uwanja wa Taifa kucheza na Ruvu Shooting huku kocha mkuu wa timu hiyo, Hans Van der Pluijm akipanga kumtumia mshambuliaji Emmanuel Okwi kwa mara ya kwanza kwenye michezo ya ligi kuu ya Bara.

Okwi hajaichezea timu hiyo mchezo wowote wa ligi tangu alipotua timu hiyo katika dirisha dogo la Januari kutokana na utata uliokuwapo kwenye usajili wake.

Afisa Habari wa klabu hiyo, Baraka Kizuguto, alisema Pluijm anaweza akamtumia Okwi leo kulingana na mahitaji yake.

"Suala la Okwi kucheza au kutocheza hilo lipo mikononi mwa kocha kulingana na kikosi chake atakachokipanga kesho," alisema Kizuguto kwa sababu "kocha kwa sasa yupo huru kumtumia na kutokana na mazoezi ya leo (jana) asubuhi ni wazi atamtumia."


Aidha, Kizuguto alisema Pluijm anajivunia ushirikiano na umoja wa wachezaji wake wanaoendelea kuuonyesha klabuni hapo.

Mashabiki wa klabu hiyo wana hamu kubwa ya kumuona kwenye ligi mshambuliaji Mganda huyo ambaye alifanya vizuri akiwa na klabu yake ya zamani ya Simba hapa nchini kabla ya kuuzwa kwa klabu ya Etoel du Sahel ya Tunisia miezi 13 iliyopita.

Yanga inavaana na Ruvu Shooting ikitokea kwenye mashindano ya kimataifa ambapo iliitoa Komorozine ya Comoro kwa jumla ya magoli 12-2 kwenye raundi ya awali ya Ligi ya Klabu Bingwa Afrika.

Van Pluijm alisema michezo ya ligi kuu ni sehemu ya maandalizi kabla ya kuvaana na mabingwa watetezi Al-Ahly ya Misri Jumamosi ijayo katika mechi ya raundi ya kwanza ya michuano hiyo ya Afrika.

Mbali na kutumia ligi kuu ya Bara kama mazoezi ya maandalizi, timu hiyo ilimtuma kocha msaidizi Charles Mkwasa Misri kushuhudia mchezo wa Super Cup kati ya Alhy na mabingwa wa Kombe la Shirikisho la klabu za Afrika CS Sfaxien ya Tunisia.

Mkwasa aliyerejea jana, alitumwa kuwasoma mabingwa mara nane hao Afrika kabla ya kuvaana nao Machi mosi.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA