MUKANGARA MGENI RASMI REDD'S MISS TANZANIA KESHO

Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Fenella Mukangara, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika shindano la urembo la taifa mwaka huu 'Redd's Miss Tanzania 2013' litakalofanyika kesho kwenye Ukumbi wa Mlimani City, Dar se Salaam.


Akizungumza jana, Mkurugenzi wa Kampuni ya Lino International Agency, Hashim Lundenga, alisema wanatarajia  kiongozi huyo wa serikali kushuhudia shindano hilo na kwamba amesharidhia kuwa mgeni rasmi.

Lundenga alisema kila kitu kimekamilika na kuwataka wadau wa sanaa ya urembo kusubiri kushuhudia shindano lililo bora zaidi ya miaka iliyopita.

"Maandalizi yamekamilika na kama ni chakula, sasa kinachosubiriwa ni kukila tu," alisema kwa kifupi mratibu huyo ambaye kampuni yake imekuwa ikiandaa shindano hilo tangu 1994.

Alisema shindano hilo litapambwa na burudani kutoka kwa mshindi wa tuzo ya mwanamuziki bora wa kike nchini, Judith Wambura 'Lady Jay Dee' ambaye kwa sasa anatamba na vibao vyake vya Yahaya na Joto Hasira, Mike Rose wa Uganda na kikundi cha ngoma za asili cha Mama Afrika.

Shindano hilo linatarajiwa kushirikisha warembo 30 kutoka sehemu mbalimbali nchini watakaowania taji linaloshikiliwa na Brigitte Alfred, kutoka Kanda ya Kinondoni jijini ambaye kwa sasa yuko Indonea akijiandaa kupanda jukwaani kuwania taji la dunia ifikapo Septemba 28, mwaka huu.

Hata hivyo, warembo watano wameshatinga hatua ya 15 bora baada ya kutwaa mataji madogo yaliyoshindanishwa wakiwa kambini.

Warembo hao ni Severina Lwinga, kutoka Chuo cha Ustawi wa Jamii jijini Dar es Salaam ambaye ni Redd's Miss Personality, Prisca Clement (Redd's Miss Tanzania Talent), Clara Bayo (Redd's Miss Sports Woman ), Happiness Watimanywa (Redd's Miss Photogenic) na Narietha Boniface ambaye ni Redd's Miss Tanzania Top Model.

Mshindi wa taji hilo mwaka huu atabeba dhamana ya kuiwakilisha nchi katika shindano la urembo la dunia mwakani na zawadi ya Sh. milioni nane pamoja na gari lenye thamani ya Sh. milioni 15.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA