HATIMAYE HAPPYNESS AMVUA TAJI BRIGITE

Happiness Watimanywa (19) (Pichani) ameung'arisha mkoa wa Dodoma na Kanda ya Kati usiku wa kuamkia jana wakati alipotwaa taji la urembo la taifa 'Redd's Miss Tanzania 2013' baada ya kuwashinda warembo wengine 29 kwenye ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.


Mrembo huyo ambaye ni mwanafunzi wa mwaka wa kwanza wa Chuo Kikuu cha Strathclyde kilichoko Glassgow, Scotland anayesomea digrii ya biashara anakuwa wa pili kutoka Dodoma kutwaa taji hilo baada ya Emily Adolph kuibuka mshindi wa taji hilo katika shindano lililofanyika mwaka 1995.

Nyota ya Happiness kutwaa taji hilo ilianza mapema akiwa kambini kwa kuwa mrembo wa kwanza kuingia hatua ya 15 bora kwa kutwaa taji la Redd's Miss Photogenic na alionekana 'kuwateka' wadau wa sanaa ya urembo kwa kushangiliwa kila alipokuwa anapita jukwaani na mavazi ya aina tatu waliyovaa warembo hao.

Akijibu swali alilochagua kuwa atafanya kitu gani tofauti endapo atashinda taji hilo ambacho hakikufanywa na warembo waliopita Happiness alisema mbali na kufanya kazi za jamii atatumia muda wake kutangaza vivutio vya utalii vyote vilivyoko Tanzania ili kuvutia wawekezaji waje kuwekeza nchini.

Mbali na kuvalishwa taji na mrembo namba mbili wa shindano hilo mwaka jana, Eugine Fabian, Happoness aliyezaliwa Morogoro alipewa zawadi ya gari jipya aina ya Toyota Vitz na jana jioni alitarajiwa kukabidhiwa Sh. milioni nane kutoka kwa wadhamini wakuu Redd's Original.

Nafasi ya pili ilichukuliwa na Latifa Mohamed kutoka Kigamboni, Kanda ya Temeke ambaye atazawadiwa Sh. milioni 6.2 wakati mshindi wa tatu ni Clara Bayo wa Ilala naye atajinyakulia Sh. milioni nne na Elizabert Pert wa Pwani (Mashariki) ataondoka na tatu huku Lucy Tomeka aliyekamilisha tano bora atazawadiwa Sh. milioni 2.4.

Warembo wengine waliofanikiwa kuingia hatua ya 15 bora ni Narietha Boniface (Redd's Miss Top Model na balozi wa Marie Stopes Tanzania), Prisca Clement (Redd's Miss Talent), Severina Lwinga (Redd's Miss Personality), Jane Awetu, Nicejack Herman, Eshy Rashid, Neema Mality, Doris Mollel, Nancy Moshi na Sabrina Juma.

Washiriki wengine 15 waliobakia ambao ni Anastazia Donald, Lina Allan, Jacquiline Luvanda, Diana Laizer, Sabra Islam, Lucy Charles, Salsha Esdory, Miriam Manyanga, Lucy James, Svetlana Nyamweyo, Glory Minja, Mary Chemponda, Philios George, Alice Isaac na Sarah Martin kila mmoja atapata kifuta jasho cha Sh. 700,000.

WAREMBO JUKWAANI

Shindano la Redd's Miss Tanzania lilianza rasmi saa 4:01 kwa warembo kupanda jukwaani wakiwa wamejigawa makundi matatu kwa kucheza shoo ya ufunguzi ya wimbo uitwao 'Personally' wa kundi la P-Square la Nigeria na kufuatia vazi la ubunifu, ufukweni yaliyobuniwa na Veronica Lugenzi na kumalizia na vazi la usiku.

LADY JAY DEE AFUNIKA

Mshindi wa tuzo ya mwanamuziki bora wa kike wa mwaka, Judith Wambura, maarufu Lady Jay Dee alifanikiwa kuwaimbisha wadau wa sanaa ya urembo waliohudhuria shindano la Redd's Miss Tanzania na kibao chake kinachotamba kiitwacho 'Yahaya'.

Jay Dee alipanda mara mbili jukwaani ambapo awali aliimba nyimbo mbili ukiwamo wa 'Joto Hasira' na aliporejea ndipo aliwasha moto kwa kuimba kibao cha 'Yahaya'.

Hata hivyo mkongwe huyo hakupanda stejini na madansa kama ilivyozoeleka katika siku za hivi karibuni kwa wasanii wa kizazi kipya kupambwa na wacheza shoo wao maalum.

Mganda, Mike Ross, alishindwa kutamba kwenye onyesho hilo huku kikundi kingine kilichotoa burudani kilikuwa ni cha sarakasi na ngoma za asili cha Mama Afrika.

Warembo wote jana jioni walitarajiwa kukabidhiwa zawadi zao za fedha katika sherehe ya kuwaaga na leo asubuhi walivunja kambi rasmi na kurejea katika familia zao.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA