GAZETI LA NIPASHE KUDHAMINI MISS TANZANIA
Gazetila NIPASHE jana lilitangaza kuwa limedhamini shindano la urembo nchini la Miss Tanzania 2013.
Simon Marwa (Pichani), Meneja wa Masoko wa Kampuni ya The Guardian Limited inayochapisha gazeti la NIPASHE, alisema NIPASHE imejitokeza kudhamini mashindano hayo kwa nia ya kusaidia kukuza sanaa ya urembo nchini.
"NIPASHE ikiwa ni moja kati ya magazeti yanayochapishwa na Kampuni ya The Guardian Limited, kwa kutambua umuhimu wa mashindano haya, imeamua kuwa moja kati ya wadhamini wa Miss Tanzania 2013 kama njia ya kukuza mashindano haya," alisema Marwa.
Aliongeza kwamba kwa kupitia udhamini huo, warembo watakaoshiriki watapata fursa ya kutambulika nchi nzima.
"Vile vile udhamini huu unalenga kuwapatia wapenzi wa urembo na mitindo burudani na matukio kemkem ambayo yatajiri katika mchakato mzima wakumpata Miss Tanzania 2013 kupitia gazeti la NIPASHE," aliongeza.
NIPASHE imekuwa mstari wa mbele kwenye kudhamini matukio tofauti nchini kama ilivyofanya katika mashindano ya Miss Tabata 2013, na Marwa alisisitiza kwamba huo ni mwanzo tu.
"Tutaendelea na mwendo huu wa kudhamini hata matukio mengine ambayo yana lengo la kuleta matokeo chanya kwenye jamii yetu," alisema.
Aidha, warembo washiriki wa Miss Tanzania 2013, kwa nyakati tofauti walimwaga tambo kuelekea kwenye fainali za mashindano hayo wakati walipokutana na waandishi wa habari kwenye hoteli ya Giraffe iliyopo Kunduchi jijini Dar es Salaam jana.
Wengi wao walionekana kujiamini zaidi na kudai wana uhakika mkubwa wa kushinda taji hilo, ambalo kwa sasa linashikiliwa na Brigette Alfred.
“Kwangu nataka kufanya kweli zaidi, kwani najua wapi naweza kuwashinda wenzangu hawa,” alisema mrembo Elizabeth Pert anayetoka mkoa wa Pwani.
Janet Awet wa Lindi naye alijisifu akisema ana sifa zote za kutwaa taji, hivyo wenzake wajiandae kuwa wasindikizaji katika shindano hilo.
Lucy Charles wa Mwanza na Esha Rashid kutoka Mara nao walitoa tambo zao, huku Severina Lwinga na Mariam Manyanga (Kanda ya Vyuo), wakitamba kwamba wao ndiyo wana uhakika wa mmojawapo kuondoka na taji.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Lino, Hashim Lundenga ambao ndiyo waandaaji wa Redd's Miss Tanzania alisema, kwa sasa kila kitu kimekamilika na anaamini warembo hao wote wana sifa zinazostahili.
“Wasichana wote waliopo hapa wana sifa za kutosha, naamini kwa dhati kabisa Redd's Miss Tanzania kwa mwaka huu atakuwa na sifa zote zinazotakiwa.”
Meneja wa Redd’s, Victoria Kimaro naye alisema, kama wadhamini wapo tayari kuhakikisha shindano hilo linafanikiwa kwa kiasi kikubwa zaidi na kumtoa mrembo bora.
“Tunaamini kabisa kama Redd’s shindano hili litatoa mrembo bora zaidi kuliko kipindi chote kwani ukiwatazama unaona wana sifa zote,” alisema.
Warembo wanaoshiriki na kanda wanazotoka zikiwa kwenye mabano ni Happiness Watimanywa (Dodoma), Sabrina Juma (Tabora), Nice-Jack Herman (Singida), Anastazia Donald (Tabora), Linah Allan (Rukwa), Jacqueliene Luvansa (Mbeya), Neema Mality (Iringa), Diana Laizer, Sabra Islam (Moro), Janet Awet (Lindi) na Elizabeth Pert (Pwani).
Wengine ni Lucy Charles (Mwanza), Esha Rashid (Mara), Salsha Isdory (Geita), Severina Lwinga, Mariam Manyanga (Kanda ya Vyuo), Lucy James (Chuo Kikuu Huria), Svetlana Nyameyo (Kurasini), Narieth James (Chang’ombe), Latifa Mohamed (Kigamboni).
Wapo pia Lucy Tomeka (Dar Indian Ocean), Prisca Clement (Sinza), Philios George (Ubungo), Sarah Martin, Dorice Mollel (Tabata), Alice Isaac na Carol Bayo (Dar City Centre).
Chanzo cha habari NIPASHE