Ruka hadi kwenye maudhui makuu

TP MAZEMBE KUMRUDISHA MBWANA SAMATTA SIMBA AGOSTI 8

SIMBA SC jana imeingia kambini Bamba Beach Hotel, Kigamboni, Dar es Salaam kujiandaa na Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, inayotarajiwa kuanza Agosti 24, mwaka huu.


Simba SC inayofundishwa na mchezaji wake wa zamani, Alhaj Abdallah Athumani Seif ‘King Kibaden’ itakuwa huko ikijifua vikali hadi itakapokuja mjini Agosti 8, kwa ajili ya kucheza mechi maalum katika Simba Day.

Bado haijajulikana Simba SC itacheza na nani Agosti 8, lakini habari za ndani zinasema Wekundu hao wa Msimbazi wanaweza kucheza na mabingwa mara nne Afrika, TP Mazembe ya DRC.

Maana yake- kama mechi hiyo itapatikana, mshambuliaji Mbwana Samatta (Pichani) wa Mazembe atacheza dhidi ya timu yake ya zamani kwa mara ya kwanza tangu ahamie DRC mwaka juzi.
   
Simba SC inaingia kambini baada ya Jumamosi kuchapwa mabao 2-1 na URA ya Uganda katika mchezo wa kirafiki Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Katika mchezo huo, uliochezeshwa na refa Michael Magori aliyesaidiwa na Iddi Likongoti na Omar Mfaume wa Dar es Salaam, hadi mapumziko Simba SC walikuwa mbele kwa bao 1-0.

Bao hilo lilifungwa na mshambuliaji mpya, Betram Mombeki aliyegongeana pasi vizuri na Marcel Boniventura. Mombeki alichukua pasi ya Singano ‘Messi’ akawapangua mabeki wa URA kabla ya kumpelekea pasi fupi Marcel aliyemrudishia mshambuliaji huyo mpya, akaunganisha nyavuni.

Baada ya kufunga bao hilo, Mombeki alikwenda kushangilia kwa staili ya mshambuliaji wa zamani wa kimataifa wa Nigeria, marehemu Rashid Yakini kwa kuingia kucheza ndani ya nyavu

Kwa ujumla Simba SC ndio waliotawala mchezo kipindi cha kwanza wakionana vema na kucheza kwa kujiamini, wakati kwa URA iliwawia vigumu kuupenya ukuta wa Wekundu wa Msimbazi, uliokuwa chini ya Mganda mwenzao, Samuel Ssenkoom, ambaye ametemwa baada ya mechi hiyo.

Kipindi cha pili, Simba SC inayofundiahwa na kocha mzalendo, Alhaj Abdallah Athumani Seif ‘King Kibadeni’ ilirudi vizuri na kuendelea kuwapa raha mashabiki wake kwa soka maridadi.

Hata hivyo, kibao kiliigeukia Simba SC baada ya mshambuliaji wake, Mombeki kutolewa kwa kadi nyekundu baada ya kumpiga kiwiko beki wa URA, Jonathan Mugabi dakika ya 51, ambaye alishindwa kuendelea na mchezo.

Baada ya hapo kwa kuwa tayari mshambuliaji mwingine aliyekuwa akiisumbua ngome ya URA, Zahor Pazi alikuwa amekwishatolewa na nafasi yake kuchukuliwa na Twaha Ibrahim, mabeki wa timu ya Uganda, wakiongozwa na Joseph Owino anayesajiliwa Simba SC baada ya mechi hiyo na Derick Walullya walianza kupanda zaidi kusaidia mashambulizi.

URA ilipata bao lake la kusawazisha dakika ya 60 mfungaji Lutimba Yayo akiunganisha krosi nzuri ya Walullya.

Wakati SImba wakijaribu kusaka bao la pili, Yayo tena akaifungia URA bao la ushindi dakika ya 75.
 
Hakukuwa tena na mashambulizi ya uhai kwa upande wa Simba na URA hawakuweza kumfunga Mganda mwenzao, Abbel Dhaira zaidi ya mara mbili.

Siku hiyo, kikosi cha Simba SC kilikuwa; Abbel Dhaira, Nassor Masoud ‘Chollo’, Issa Rashid ‘Baba Ubaya’, Rahim Juma/Sino Augustino, Samuel Ssenkoom, Jonas Mkude, Ramadhani Singano/Miraj Adam, William Lucian, Betram Mombeki, Zahor Pazi/Twaha Ibrahim na Marcel Boniventura.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

FIFA yatoa orodha ya vilabu bora duniani, Simba na Yanga zachuana vikali

SHIRIKISHO la Soka Afrika (CAF) limetoa orodha ya viwango vya ubora wa klabu barani, Simba ikiendelea kuwa juu ya klabu nyingine za Tanzania, nafasi ya tano. Orodha hiyo imetoka leo kuelekea droo ya hatua za awali za michuano ya klabu Afrika ambayo kwa mara ya kwanza kihistoria itafanyika nchini katika studio za Azam Tv, Tabata Jijini Dar es Salaam. Yanga ambayo kama Simba itashiriki Ligi ya Mabingwa — yenyewe inashika nafasi ya 12, wakati timu nyingine katika orodha hiyo ni Namungo FC wanaoshika nafasi ya mwisho, ya 75 kwa pamoja na Salitas FC ya Burkina Faso, Ahli Benghazi ya Libya na NAPSA Stars ya Zambia. Kwa msimu ujao mbali na Simba na Yanga kushiriki Ligi ya Mabingwa, Azam FC na Singida Black Stars zitashiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

Timu inaitwa Mashujaa Lake Tanganyika FC ( Mashujaa FC ) ilianza rasmi kampeni yake ya kupanda Ligi Kuu tarehe 29/9/2018 na imepanda Ligi Kuu 25/06/2023 miaka mitano ya kupambana kwenye Ligi Daraja la kwanza Championship. Timu hii inaendeshwa kwa ushirikiano wa pande mbili kati ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji kwa niaba ya Wananchi wa Kigoma. Muelewe hapa maana wengi wanasema ni timu ya Jeshi asilimia 100% Nembo ya timu ni Sokwe Dume, Shujaa wa Hifadhi za Gombe na Mahale zilizopo mkoani Kigoma. Rangi ya kwanza ya jezi ya timu (first kit) ni hiyo hapo chini na kwenye nembo ya timu ni rangi za tunda la michikichi (mawese ). Hii kama njano ni mawese yaliyoganda na huo wekundu ni mawese ya moto. Ukishika tunda la Mse juu utaona wekundu na ukikata katikati utaona njano. Nyeupe ni ‘nazi’ ya Mse hizi ni alama za utajiri wa Kigoma Jezi nyingine ni blue inayowakilisha Ziwa Tanganyika na Jezi nyingine ni Nyeupe

Beno Ngassa mdogo wa Mrisho Ngassa anayekipiga Tanzania Prisons

Miongoni mwa viungo wa pembeni wanaofanya vizuri ni Benodict Khalfan Ngassa ambaye amekuwa akifanya vizuri. Ngassa ambaye ni mtoto wa mchezaji wa zamani wa Pamba Jiji na Simba SC, Khalfan Ngassa, pia ni mdogo wa kiungo mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Simba na Azam, Mrisho Ngassa anatajwa ni mmoja kati ya wachezaji wanaotazamiwa kufanya makubwa siku za usoni. Mambo Uwanjani Blog itawaletea Makala maalum ya kiungo huyo hatari ambaye ndoto zake ni kufuata nyayo za kaka yake Mrisho Ngassa. Beno Ngassa