GOR MAHIA YAZIDI KUPETA KENYA

Teddy Akumu 

Gor Mahia walipanua pengo kati yao na wapinzani wao kileleni mwa Ligi Kuu ya Kenya kwa ushindi wa 2-1 dhidi ya Karuturi Sports kwenye mechi iliyochezewa uwanja wa City mnamo Jumamosi.

Mechi hiyo ilianza kwa mwendo wa kasi sana ikihusisha timu iliyo juu ligini na iliyo chini.
Paul Mungai Kiongera na Innocent Mutiso ndio waliotamba zaidi upande wa Gor Mahia kipindi cha kwanza na walifanikiwa kutumia kasi ya mchezo kufanya mashambulio makali upande wa Karuturi.
Mashambulio hayo yaliumiza Karuturi dakika ya tatu huku Samuel Kariuki akiadhibiwa na refa kwa kumchezea visivyo Erick Ochieng’.
Joseph Njuguna alipoteza nafasi ya mwaka huku kombora lake likiokolewa na Ayuko kwa kutumia miguu yake kunako dakika ya 12.
Gor walijipata kifua mbele dakika ya 17 baada ya Omondi kutuma wavuni mpira ulioandaliwa na Kiongera ambaye alikuwa amempokonya mpira Emmanuel Olupot.
Karuturi, hata hivyo, walijikwamua na wakaanza kufufuka kupitia kasi ya John Kiplangat aliyeshirikiana vyema na kifaa kutoka Uganda Zzinda Hussein.
Fowadi huyo wa zamani wa Gor, Kiplangat, alifanya mambo dakika ya 32 – na kumlazimisha kipa Jerim Onyango kufanya kazi ya ziada kuokoa kombora lake upande wa kulia.
Jeraha lililompata Eric Ochieng, hata hivyo lilimlazimisha kocha Bobby Williamson kufanya badiliko lake la kwanza huku difenda kutoka Uganda Ivan Anguyo akiingia uwanjani.
Kipindi cha pili kilikuwa na visa zaidi kwani kila upande ulijizatiti kudhibiti mchezo, lengo likiwa kufunga mabao. Karuturi hapo walifunga bao lililoonekana kuwa la utata na kusawazisha kupitia kifaa kutoka Uganda Zzinda Hussein kunako dakika ya 50 baada yake kuonekana kana kwamba alikuwa ameotea.
Zzinda alituliza mpira kwa kutumia kifua eneo la hatari na kisha akautuma nyuma ya Jerim Onyango aliyekuwa akimkaribia.
Mchezo ulisimamisha karibu dakika tano baada ya wachezaji wa Gor Mahia kulalamikia hatua ya refa mkuu na mtunza mstari ya kuruhusu bao hilo lakini lilibaki.
Gor baadaye waliwatia presha Karuturi baada ya mchezo kuanza huku mafowadi wake wakifanya mashambulio makali na kuwafanya mashabiki wa Karuturi wakose kutulia kwenye viti vyao.
Israel Emuge baadaye aliwarejeshea Gor Mahia uongozi kunako dakika ya 70, kwa kufunga mpira wa kichwa kutoka kwa mkwaju wa adhabu uliotwangwa na Innocent Mutiso ambao ulikuwa umesababisha mtafaruku karibu na goli.
Karuturi hawakuweza kujikwamua licha ya refa kuongeza dakika nane za ziada kwani Gor walikwamilia uongozi na wakasonga hadi alama saba mbele ya Thika United kwenye jedwali.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA