MWANZO WA AFRIKA -3
Inaandikwa na Fikiri Salum
Ilipoishia
WAJERUMANI nao wakachukuwa Togoland, Cameroon na baadhi ya nchi katika Afrika ya magharibi na Afrika ya mashariki, lakini baada ya vita vya kwanza vya dunia wakanyang' anywa.
Endelea
Waitalia wakachukuwa Libya, Eritrea na sehemu kubwa ya Somalia.
UHURU WA AFRIKA
Nchi ya kwanza kujitawala upya katika Afrika ni nchi ya Afrika Kusini zilizojiunga na kujiendesha wao wenyewe katika mwaka 1910, Misri, katika mwaka 1922 walikuwa wanajiendesha wenyewe, na Tongier katika mwaka wa 1925.
Madola mengi ya Afrika yalianza kupigania uhuru katika miaka ya baina ya 1950 na 1960, na Wazungu wakasalimu amri na kuanza kutoa uhuru.
Libya wakajinyakulia uhuru katika mwaka wa 1951, Eritrea katika mwaka 1952 ikiwa imejiunga na Ethiopia, Morocco katika mwaka 1956 na wakarudishiwa Tongier.
Katika mwaka wa 1960:Ufaransa ukatoa uhuru kwa Cameroon, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Chad, Kongo Brazzaville, Cote D Ivoire, Dahomey (Benin), Gabon, Madagascar, Mali, Mauritania, Niger, Senegal, na Volta ya juu (Burkina Faso) zikapewa uhuru .
Vilevile katika mwaka huu huo wa 1960, Congo (Kinshasa), Nigeria, Somalia, na Togo zikapata uhuru na katika mwaka wa 1961, Sierra Leone na Tanganyika zikapata uhuru na Afrika ya Kusini ikawa Jamhuri.
Katika mwaka wa 1962 Algeria, Burundi, Rwanda, na Uganda zikawa huru na 1963 zikafuatia Zanzibar, Gambia na Kenya na katika mwaka wa 1964 Malawi (Nyasaland) na Zambia (Rhodesia ya kaskazini) zikapata uhuru.
Baada ya miaka miwili katika mwaka wa 1966 Botswana (Bechuanaland) na Lesotho (Basutoland) zikajinyakulia uhuru, Mauritius na Swaziland katika mwaka 1968 na vilevile Guinea ya Ikweta, Hispania ikairudishia Ifni katika mwaka wa 1969 katika mamlaka ya Morocco.
Aidha, katika mwaka wa 1974 Guinea ya Kireno (Guinea Bissau) ikapata uhuru wake, na katika mwaka wa 1975 Angola, Cape Velde, Msumbiji, Sao Tome na Principe zikapata uhuru.
Hispania vilevile ikaitoa Sahara ya magharibi kwa Morocco na Mauritania katika mwaka wa 1976, lakini wananchi wakakataa kuwa chini ya nchi mbili hizi, kukazuka vita, Mauritania ukaitoa sehemu yake na kuipa Morocco katika mwaka 1979, tatizo ambalo mpaka sasa linaendelea baina ya Morocco na Sahara ya magharibi na Umoja wa mataifa (UN) unajaribu kutatua tatizo hili.
Waingereza wakaipa uhuru Shelisheli katika mwaka wa 1976 na Ufaransa ukatoa uhuru kwa visiwa vya Ngazija (Comoro).
Katika mwaka 1977 Djibouti (nchi ya Afars na Issas) iliyokuwa ikitawaliwa na Ufaransa ikarudi kwa wenyewe, Rhodesia (Zimbabwe) ikapata uhuru halisi mwaka 1980, na South West Africa iliyokuwa ikitawaliwa na Afrika Kusini ikapata uhuru katika mwaka 1990 na kuitwa Namibia.
Uingereza umebaki na visiwa vya Saint Helena na Ascension na Ufaransa unaendelea kutawala Mayotte na Reunion, Hispania vilevile unaendelea kutawala visiwa vya Canarias pamoja na Ceuta na Melina na visiwa vingine vilivyoko karibu na Morocco .
MWISHO
