Rais mstaafu Dkt. Jakaya Kikwete, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jopo la Wazee la Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika, amekutana na timu ya mpira wa kikapu ya Dar City inayoshiriki Michuano ya Ligi ya Mpira wa Kikapu Afrika 2026, inayoendelea jijini Pretoria, Afrika Kusini.
Katika mazungumzo hayo, yaliyoihusisha pia timu hiyo pamoja na Rais wa Shirikisho la Mpira wa Kikapu Tanzania (TBF), Hasheem Thabit, na viongozi wengine wa Serikali, Dkt. Kikwete ameipongeza Dar City kwa kufikia hatua hiyo muhimu, akieleza kuwa mafanikio hayo yanaashiria kukua kwa kiwango cha mpira wa kikapu nchini Tanzania.
Aidha, amewatia moyo wachezaji wa Dar City kupambana katika mchezo wao unaofuata Machi 31, 2026, akisisitiza umuhimu wa nidhamu, kujituma na kujiamini wanapoingia uwanjani.
“Kwa hatua mliyofikia, nina imani kabisa mnaweza kutinga fainali na hatimaye kubeba kombe hili,” amesema Dkt. Kikwete.
Dkt. Kikwete yupo nchini Afrika Kusini kwa ziara ya kikazi, ambapo pia amekutana na Rais Cyril Ramaphosa, ikiwa ni sehemu ya kutekeleza majukumu yake ya kikanda pamoja na jukumu lake chini ya Umoja wa Afrika la kusaidia kutafuta suluhu ya mgogoro wa Sudan Kusini.

