YANGA YAMALIZANA NA STRAIKA LA PLATINUM YA ZIMBABWE
Katika kuhakikisha inafanya vizuri katika msimu ujao wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara pamoja na mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, uongozi wa Yanga umesema umemalizana na mshambuliaji wa Platinum FC ya Zimbabwe, Donald Ngoma, baada ya kukubaliana kusaini mkataba wa miaka miwili. Kwa mujibu wa habari zilizopatikana kutoka ndani ya uongozi wa Yanga tayari wamekamilisha mazungumzo na mchezaji huyo na anatarajiwa kutua nchini mapema mwezi ujao kumaliza taratibu zilizobaki na kisha kuungana na kikosi cha mabingwa hao wa Bara ambacho kitaanza mazoezi Juni 8, mwaka huu. Chanzo hicho kiliendelea kueleza kuwa wanaamini uwezo wa mshambuliaji huyo wa timu ya Taifa ya Zimbabwe utasaidia kuimarisha safu ya ushambuliaji baada ya Mrisho Ngasa kuondoka. "Hapa ninavyozungumza na wewe huyo mchezaji ni mali ya Yanga tayari, tumeshamalizana naye, tumempa mkataba wa miaka miwili," alisema kiongozi huyo wa juu wa Yanga.