Nooij: Stars fiti kuivaa Swaziland leo.

Timu ya Soka ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars), leo inatarajiwa kushuka katika Uwanja wa Olympia Park, Rustenburg Afrika Kusini kuvaana na Swaziland katika michuano ya Baraza la Vyama vya Soka Kusini mwa Afrika (Cosafa).

Tanzania itashuka uwanjani katika mechi hiyo ya Kundi B, itakayopigwa majira ya saa 2:00 usiku kwa saa za Afrika Mashariki ikiwa kama nchi alikwa kwenye michuano hiyo.

Kocha Mkuu wa timu ya Taifa Stars, Mart Nooij, amesema kuwa wachezaji wake wako tayari kwa mchezo huo baada ya kufanya mazoezi kwa siku zote walizokuwa huko licha ya hali ya hewa ya kuwa ya baridi kali.


Nooij alisema wachezaji wake walitarajiwa kufanya mazoezi ya mwisho jana jioni kwa lengo la kujiandaa kuikabili Swaziland na kwamba wote wapo fiti.

"Hakuna mchezaji ambaye ameshindwa kufanya mazoezi licha ya hali ya hewa ya baridi, kila mmoja anajituma, ni dalili njema ndani ya timu kwa sababu tunahitaji kupata matokeo mazuri," alisema Kocha huyo.

Taifa Stars ambayo ni timu alikwa kwenye michuano hiyo inayofanyika kila mwaka itashuka tena Jumatano Mei 20 mwaka huu kuivaa Madagascar na itamaliza mechi zake za hatua ya makundi Ijumaa kwa kucheza na Lesotho.

Mshindi wa kila kundi ataungana na wenyeji Afrika Kusini, Msumbiji, Zambia, Ghana, Botswana na Malawi kucheza hatua ya robo fainali.

Kutakuwa na nusu fainali za aina mbili, kwanza za timu zilizofungwa katika robo fainali na zilizoshinda kwenye hatua hiyo.

Pia timu vibonde zitaendelea kupepetana hadi fainali yao ambayo itapigwa Mei 29, wakati fainali ya wakali itakuwa Mei 30.

Baada ya kumaliza mashindano hayo, Taifa Stars itaendelea na mazoezi kwa ajili ya mechi zake mbili zinazofuata dhidi ya Misri (mechi za mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika- Afcon) na baadaye Uganda kwenye michuano ya kuwania tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN).

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA