YANGA YAMALIZANA NA STRAIKA LA PLATINUM YA ZIMBABWE

Katika kuhakikisha inafanya vizuri katika msimu ujao wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara pamoja na mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, uongozi wa Yanga umesema umemalizana na mshambuliaji wa Platinum FC ya Zimbabwe, Donald Ngoma, baada ya kukubaliana kusaini mkataba wa miaka miwili.

Kwa mujibu wa habari zilizopatikana kutoka ndani ya uongozi wa Yanga tayari wamekamilisha mazungumzo na mchezaji huyo na anatarajiwa kutua nchini mapema mwezi ujao kumaliza taratibu zilizobaki na kisha kuungana na kikosi cha mabingwa hao wa Bara ambacho kitaanza mazoezi Juni 8, mwaka huu.

Chanzo hicho kiliendelea kueleza kuwa wanaamini uwezo wa mshambuliaji huyo wa timu ya Taifa ya Zimbabwe utasaidia kuimarisha safu ya ushambuliaji baada ya Mrisho Ngasa kuondoka.

"Hapa ninavyozungumza na wewe huyo mchezaji ni mali ya Yanga tayari, tumeshamalizana naye, tumempa mkataba wa miaka miwili," alisema kiongozi huyo wa juu wa Yanga.


Aliongeza kuwa usajili wa mwaka huu utafanyika kwa mapendekezo ya kocha na hakutakuwa na mchezaji atakayeletwa na kiongozi au mwanachama yeyote wa timu hiyo.

"Tuliahidi kuiboresha Yanga, tutafanya kila kitu kisasa kulingana na taratibu zinazostahili, kwa upande wa usajili, mwalimu ndiye anajua ubora wa timu na mapungufu yaliyoko, yeye ndiye atasema nani asajiliwe au aachwe," aliongeza.

Ngoma jana jioni alitarajiwa kuiongoza safu ya ushambuliaji ya Zimbabwe dhidi ya Mauritius kwenye mashindano ya Kombe la Cosafa yanayofanyika Afrika Kusini kwa kushirikisha timu mbalimbali za Ukanda wa Kusini mwa Afrika, Tanzania ikiwa mojawapo kama nchi alikwa.

Mbali na nyota huyo, tayari Yanga imeshamnasa Mwinyi Haji Mngwali wa KMKM ya Zanzibar ambaye kwa sasa ameitwa katika kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) kilichoko Afrika Kusini.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA