SIMBA YAIFANYIA UMAFIA MKUBWA YANGA, YAMPORA STRAIKA NA KUMWAGA WINO.

Katika kuhakikisha kikosi cha Simba kinarejesha makali yake kwenye msimu ujao wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara, uongozi wa timu hiyo umefanikiwa kunasa saini ya mshambuliaji wa timu ya Taifa ya Kenya (Harambee Stars), Paul Kiongera.

Kwa mujibu wa habari zilizopatikana jijini kutoka katika kamati ya usajili ya timu hiyo, Kiongera, ambaye ni mchezaji wa KCB inayoshiriki Ligi Kuu ya Soka ya Kenya, amesaini mkataba wa miaka miwili.

Chanzo hicho kilisema kuwa kwa sasa Kiongera ni mmoja wa washambuliaji wanaoaminiwa na kocha mkuu wa Harambee Stars, Adel Amrouche na vile vile Kocha Mkuu wa Simba, Mcroatia Zdravko Logarusic, anatambua uwezo wake.


"Tayari wameshamalizana na Kiongera," kilisema chanzo chetu.Kiongozi huyo alisema mshambuliaji huyo anatarajiwa kuwasili nchini siku yoyote kuanzia keshokutwa ili kukamilisha taratibu nyingine za usajili.

Habari zaidi kutoka Simba zinaeleza kuwa bado mazungumzo na kiungo wa zamani wa timu hiyo, Jerry Santo, ambaye aliichezea Coastal Union hayajakamilika.

"Santo bao, kuna vitu wanaviangalia kwanza halafu watafikia maamuzi," aliongeza.Wakati huo huo, Logarusic anatarajiwa kurejea nchini leo jioni akitokea kwao Croatia ambako alikua likizo baada ya msimu uliopita wa Ligi Kuu ya Bara kumalizika.

Mara baada ya kurejea nchini, Logarusic, anatarajiwa kukutana na uongozi mpya wa klabu hiyo ulioingia madarakani hivi karibuni kwa ajili ya kufanya mazungumzo na hatimaye kusaini mkataba mpya wa kukinoa kikosi cha Wekundu wa Msimbazi.

Logarusic ambaye alitua nchini mapema Desemba mwaka jana na kurithi mikoba ya Abdallah King Kibaden, alipewa mkataba mfupi wa miezi sita ambao ulimalizika Mei 31, mwaka huu.

Simba inatarajia kuondoka nchini Julai 20, mwaka huu kuelekea Afrika Kusini kwa ajili ya kuweka kambi maalumu ya kujiandaa na msimu ujao wa ligi ambayo itaanza Agosti 24.

Kikosi hicho kinatarajiwa kuweka kambi ya siku 17 katika jiji la Johannesburg na mara baada ya kurejea itacheza mechi ya utambulisho wa kikosi chao itakayofanyika Agosti 8, mwaka huu katika tamasha maalum la 'Simba Day'.

Mbali na Simba, timu nyingine ambazo zinajiandaa na ligi hiyo ni pamoja na bingwa mtetezi Azam, Yanga, Mtibwa Sugar, Kagera Sugar, Mbeya City, Prisons, JKT Ruvu, Ruvu Shooting, JKT Mgambo, Coastal Union, Ndanda FC, Stand United na Polisi Morogoro.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA