Ruka hadi kwenye maudhui makuu

MALINZI AWASUTA MAREFA WA TANZANIA, ADAI WAMESHAMIRI RUSHWA

RAIS wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi amesema kwamba sekta ya marefa nchini inatia aibu kwa sababu ipo chini mno na amewataka viongozi wa sekta hiyo kuhakikisha wanaiinua juu.

Akizungumza wakati wa kufunga semina ya marefa wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Malinzi amesema kwamba ipo haja ya jitihada kubwa kufanyika kuinua sekta hiyo.


Malinzi amesema baadhi ya nchi jirani ikiwemo Kenya zilikuwa na marefa katika Kombe la Dunia mwaka huu nchini Brazil, lakini Tanzania haikuwa na refa hata mmoja.Amesema hata kwenye michuano mingine ya barani, kama Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) bado ushiriki wa marefa wa Tanzania ni duni.

Malinzi ameshauri vyuo vya elimu ya juu nchini navyo visaidie kutoa mafunzo ya urefa, akitolea mfano Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ambao wana somo la Elimu ya Viungo inayohusu mwili wa mwanamichezo (PE).

“Mfano pale UD (Chuo Kikuu Dar es Salaam) wana somo la PE, kama wataamua kutoa mafunzo ya urefa sisi (TFF) tutakuwa tayari kuwapa ushirikiano ili kuhakikisha tunainua viwango vya marefa nchini,”amesema Malinzi.

Malinzi amesema kwamba amesikitishwa na mkoa wa Ruvuma alipoutembela hivi karibuni na kukuta una marefa wanane tu, wakati ni mkubwa na una wilaya nyingi.
 “Nilishangaa sana, mkoa mkubwa kama ule una marefa wanane tu, sasa huyo bingwa wa mkoa anapatikana vipi, kwa kweli hali ni mbaya sana,”amesema.

Malinzi amesema baada ya hali hiyo, ameagiza TFF ifanye tathmini ya kujua kila mkoa una marefa wangapi ili kujua sehemu ambazo wana mapungufu waelekeze nguvu ya kuinua marefa.

Amesema ipo haja ya waamuzi wastaafu, wakongwe na viongozi wa marefa kushirikiana kuinua marefa chipukizi katika viwango vizuri ili taifa liwe na marefa wa kutosha siku za usoni.

Pamoja na hayo, Malinzi amewaasa marefa kujiepusha na rushwa- kwani soka ya Tanzania kwa sasa inanyemelewa na maharamia wa kimataifa wa kupanga matokeo ili kujinufaisha katika mchezo wa kamari.

“Nina ushahidi wa kutosha mechi za Tanzania sasa zinachezewa kamari nje ya nchi, sasa hii ni hatari sana kwa soka yetu, naomba sana mjiepushe na upangaji wa matokeo,”amesema.

Malinzi amesema TFF inawafanyia uchunguzi marefa wawili kwa tuhuma za kupanga matokeo ambao kwa sasa wamesimamishwa ili kupisha uchunguzi huo, na ikibainika ni kweli watachukuliwa hatua kali za kisheria.

“Nchi za wenzetu ukigundulika ulihusika na upangaji wa matokeo, unapelekwa mahakamani sheria inafuata mkondo wake, sasa na sisi tutafanya nini, kwa hiyo naomba sana tujiepushe na upangaji wa matokeo,”Malinzi aliwaambia marefa huyo.

Semina hiyo iliendeshwa na mkufunzi wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), Carlos Henriuques kutoka Afrika Kusini ambaye ni Ofisa Maendeleo ya Marefa wa shirikisho hilo.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

FIFA yatoa orodha ya vilabu bora duniani, Simba na Yanga zachuana vikali

SHIRIKISHO la Soka Afrika (CAF) limetoa orodha ya viwango vya ubora wa klabu barani, Simba ikiendelea kuwa juu ya klabu nyingine za Tanzania, nafasi ya tano. Orodha hiyo imetoka leo kuelekea droo ya hatua za awali za michuano ya klabu Afrika ambayo kwa mara ya kwanza kihistoria itafanyika nchini katika studio za Azam Tv, Tabata Jijini Dar es Salaam. Yanga ambayo kama Simba itashiriki Ligi ya Mabingwa — yenyewe inashika nafasi ya 12, wakati timu nyingine katika orodha hiyo ni Namungo FC wanaoshika nafasi ya mwisho, ya 75 kwa pamoja na Salitas FC ya Burkina Faso, Ahli Benghazi ya Libya na NAPSA Stars ya Zambia. Kwa msimu ujao mbali na Simba na Yanga kushiriki Ligi ya Mabingwa, Azam FC na Singida Black Stars zitashiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Beno Ngassa mdogo wa Mrisho Ngassa anayekipiga Tanzania Prisons

Miongoni mwa viungo wa pembeni wanaofanya vizuri ni Benodict Khalfan Ngassa ambaye amekuwa akifanya vizuri. Ngassa ambaye ni mtoto wa mchezaji wa zamani wa Pamba Jiji na Simba SC, Khalfan Ngassa, pia ni mdogo wa kiungo mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Simba na Azam, Mrisho Ngassa anatajwa ni mmoja kati ya wachezaji wanaotazamiwa kufanya makubwa siku za usoni. Mambo Uwanjani Blog itawaletea Makala maalum ya kiungo huyo hatari ambaye ndoto zake ni kufuata nyayo za kaka yake Mrisho Ngassa. Beno Ngassa

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

Timu inaitwa Mashujaa Lake Tanganyika FC ( Mashujaa FC ) ilianza rasmi kampeni yake ya kupanda Ligi Kuu tarehe 29/9/2018 na imepanda Ligi Kuu 25/06/2023 miaka mitano ya kupambana kwenye Ligi Daraja la kwanza Championship. Timu hii inaendeshwa kwa ushirikiano wa pande mbili kati ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji kwa niaba ya Wananchi wa Kigoma. Muelewe hapa maana wengi wanasema ni timu ya Jeshi asilimia 100% Nembo ya timu ni Sokwe Dume, Shujaa wa Hifadhi za Gombe na Mahale zilizopo mkoani Kigoma. Rangi ya kwanza ya jezi ya timu (first kit) ni hiyo hapo chini na kwenye nembo ya timu ni rangi za tunda la michikichi (mawese ). Hii kama njano ni mawese yaliyoganda na huo wekundu ni mawese ya moto. Ukishika tunda la Mse juu utaona wekundu na ukikata katikati utaona njano. Nyeupe ni ‘nazi’ ya Mse hizi ni alama za utajiri wa Kigoma Jezi nyingine ni blue inayowakilisha Ziwa Tanganyika na Jezi nyingine ni Nyeupe