Makamu wa Rais Yanga awatoa hofu kuhusu uwanja Jangwani

Makamu wa Rais wa klabu ya Young Africans (Yanga SC), Arafat Haji, amewatoa hofu mashabiki na wanachama wa klabu hiyo kuhusu mradi wa ujenzi wa uwanja wao wa kisasa eneo la Jangwani, kwa kueleza kuwa tayari wameshasaini mkataba rasmi na mwekezaji GSM tangu tarehe 12 na mchakato wa maandalizi unaendelea vizuri.

Ametoa ufafanuzi kuwa sababu ya kutooana ujenzi wa moja kwa moja ukiendelea eneo la tukio ni kutokana na kuwepo kwa miradi mingine inayotegemeana kama mradi wa Mto Msimbazi na daraja jipya, huku vifaa vya uwanja huo vikiwa vinaandaliwa na kuunganishwa huko vinakotoka.

Arafat aliongeza kuwa uwanja huo utatumia teknolojia ya kisasa na hautakuwa wa zege tupu, bali vifaa vingi vitaletwa kutoka nje ya nchi na kuunganishwa mahali hapo baada ya kukamilisha kujaza eneo hilo ili kufikia kiwango na urefu ulioshauriwa na wataalamu wa Bonde la Jangwani.

Hatua hiyo inachukuliwa kwa umakini mkubwa ili kuepuka changamoto za mafuriko na athari za maji ya mvua, huku wakihakikisha ujenzi unafuata misingi yote ya kitaalamu.

Mwisho, Makamu huyo wa Rais amebainisha kuwa mradi huo utakuwa alama na urithi mkubwa kwa viongozi wa sasa na mwekezaji GSM kwa kukubali kuwekeza fedha zao.

Lengo kuu la uongozi huo ni kuhakikisha kuwa ndani ya miaka minne ijayo wanaondoka madarakani wakiwa wameiachia Yanga uwanja mpya na wa kisasa, ambao hautakuwa tu fahari kwa Wananchi bali pia utakuwa chanzo endelevu cha mapato kwa klabu hiyo.