Kagame Cup kulamba milioni 79
Klabu ya Al Hilal ya nchini Sudan imechukua hatua kubwa na ya kihistoria baada ya kujitolea kudhamini michuano ya Kombe la CECAFA Kagame Cup 2026 kwa kutoa kiasi cha dola za Kimarekani laki moja ($100,000), ambazo ni zaidi ya Shilingi Milioni 263 za Kitanzania.
Kwa mujibu wa taarifa za ndani, miamba hiyo ya soka ya Sudan imekubali kutoa mkono huo wa heri ili kufanikisha uendeshaji wa mashindano hayo yanayotarajiwa kurindima hivi karibuni nchini Rwanda.
Lengo kuu la Al Hilal kuingia kama mdhamini mkuu ni kuyatumia mashindano hayo adhimu ya ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kama sehemu ya maandalizi yao ya msimu mpya (Pre-Season).
Klabu hiyo inataka kupima makali ya kikosi chake dhidi ya timu pinzani ili kujiweka sawa kuelekea mashindano ya ndani na yale ya kimataifa, huku ikiongeza chachu na mvuto wa kiushindani katika michuano hiyo.
Kufuatia udhamini huo mnono, mchanganuo wa zawadi zitakazotolewa kwa timu zitakazofanya vizuri umebadilika na kuwa wa kuvutia zaidi.
Bingwa mpya wa michuano hiyo ataondoka na kitita cha dola 30,000 (takriban Tsh Milioni 79), huku mshindi wa pili akijinyakulia dola 20,000 (takriban Tsh Milioni 52) na mshindi wa tatu atazawadiwa dola 10,000 (takriban Tsh Milioni 26).
