Yanga bingwa Ligi Kuu bara, yarudia historia ya mwaka 1968-1972
TIMU ya Yanga imefanikiwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara baada ya ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya JKT Tanzania jioni ya leo Uwanja wa Meja Jenerali Charles Isamuhyo, Mbweni, Dar es Salaam.
Mabao ya Yanga SC leo yamefungwa na mshambuliaji Mzimbabwe, Prince Mpumelelo Dube dakika ya nane, kiungo Maxi Mpia Nzengeli kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na mshambuliaji Laurindo Dilson Maria AurĂ©lio ‘Depu’ kutoka Angola dakika ya 66.
Kwa ushindi huo, Yanga SC inamaliza Ligi Kuu msimu wa 2025 – 2026 ikiwa na pointi 75, mbili Zaidi ya watani wao, Simba SC waliomaliza nafasi ya pili baada ya ushindi wa 1-0 dhidi ya wenyeji, KMC FC jioni ya leo Uwanja wa KMC Complex, Mwenge, Dar es Salaam.
Hilo linakuwa taji la tano mfululizo la Ligi Kuu kwa Yanga kuanzia msimu wa 2021–2022, 2022–2023, 2023–2024 na 2024–2025 na hiyo inakuwa mara ya pili kwa wana Jangwani hao kutwaa mataji ya Ligi Kuu mara tano mfululizo baada ya kufanya hivyo misimu ya 1968, 1969, 1970, 1971 na 1972.
Kwa ujumla hilo linakuwa taji la 32 la ubingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara kwa Yanga – pamoja na yale iliyobeba kwenye misimu ya 1974, 1981, 1983, 1987, 1991, 1996, 1997, 2000, 2005, 2006, 2008, 2009, 2011, 2012–2013, 2014–2015, 2015–2016 na 2016–2017.
Timu nyingine iliyowahi kutwaa taji la Ligi Kuu mara tano mfululizo ni watani wao, Simba SC waliofanya hivyo mara moja kuanzia msimu wa 1976, 1977, 1978, 1979 na 1980, ambao pia wanafuatia kwa kutwaa mataji mengi ya Ligi Kuu kwa ujumla, 22 mengine miaka ya 1965, 1966, 1973, 1993, 1994, 1995, 2001, 2002, 2003, 2004, 2007, 2009–2010, 2011–2012, 2017–2018, 2018–2019, 2019–2020 na 2020–2021.
