Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. CPA. Amos Gabriel Makalla, rasmi amekubali kuwa Mlezi wa Timu ya mpira wa Miguu ya Mbuni FC yenye Makao yake Makuu Mkoani humo, kufuatia ombi lililowasilishwa kwake na JWTZ Brigedi ya Kanda ya Kaskazini.
CPA. Makalla ameanza ulezi huo rasmi leo Oktoba 23,2025, alipokutana na kuzungumza na Menejimenti na Wachezaji wa timu hiyo na kutoa shilingi milioni 13.5 kwa ajili ya posho na motisha kwa wachezaji huku akiwataka kuanza safari ya kuipandisha timu hiyo ili kucheza Ligi kuu, kama sehemu ya kukuza utalii wa Michezo Arusha.
Aidha, CPA Makalla ametoa vyakula na televisheni kwaajili ya kambi ya timu hiyo huku Uongozi wa Timu hiyo ukimshukuru kwa motisha na kukubali kuwa mlezi wa timu hiyo, na kuahidi ushindi kwa michezo ijayo.
Awali, CPA Makalla ameitaka timu hiyo kuweka malengo ya kushinda mechi zote za nyumbani, na kusisitiza kuwa Serikali ya awamu ya sita inajenga viwanja vya michezo pamoja na uwanja wa kisasa wa mpira wa miguu, ikiwa ni maandalizi ya michuano ya soka barani Afrika AFCON 2027.