Simba hawalazi damu
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally, ameweka wazi kuwa kikosi chao hakina muda wa kupoteza ambapo mara baada ya ushindi mnono dhidi ya Mtibwa Sugar, timu hiyo ilisafiri usiku huohuo kutoka Morogoro kurejea Dar es Salaam kwa ajili ya kuingia kambini moja kwa moja.
Simba sasa inaelekeza nguvu zote kwenye mchezo wa raundi ya 29 wa Ligi Kuu ya NBC dhidi ya Singida Black Stars, mtanange utakaopigwa Jijini Dar es Salaam kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo kuanzia saa 10:00 jioni.
Ahmed amefunguka kuwa kwa sasa klabu hiyo imeweka pembeni mpango wa kucheza soka la kuvutia au kuonyesha mbwembwe uwanjani, bali nguvu zote zimeelekezwa kwenye kusaka alama tatu muhimu pekee
Aliongeza kuwa mbinu hiyo ya kucheza soka la moja kwa moja (direct football) ilianza kutumika tangu raundi ya 25 kutokana na mazingira magumu ya viwanja vya mikoani kama Jamhuri, pamoja na ukweli kwamba wanakutana na timu zinazopambana kufa na kupona kujinasua kutoka janga la kushuka daraja.
Kuelekea mchezo huo, msemaji huyo ametoa wito mzito kwa mashabiki na wanachama wa Simba kudumisha utulivu na umoja, huku akiwataka kuacha kabisa kufuatilia matokeo au mambo yanayofanywa na wapinzani wao wakubwa (Yanga SC).
Ahmed amesisitiza kuwa jambo la msingi kwao kwa sasa ni kuona timu yao inashinda michezo yote iliyobaki, na baada ya hapo ndipo watakapokaa chini na kuangalia mahesabu ya msimamo wa ligi yanasomeka vipi.

