UKRISTO NI CHIMBUKO LA UYAHUDI - 13
Inaandikwa na Fikiri Salum
Ilipoishia
KUHUSU maeneo ambako Wakristo wanapungua ni kwamba kutokana na historia ya kanisa kuwa na mchanganyiko wa mazuri na mabaya, wengine wanahisi kuwa halina maana tena.
Endelea
Pia Kuna makundi kama Wakomunisti na Wamasoni ambayo yanakusudia kabisa kufuta Ukristo kwa kutangaza kasoro za waumini na viongozi wao, pamoja na kuhimiza watu kwenda kinyume cha maadili.
Hali hii inajionyesha hasa pale ambapo waamini wengi, hasa Ulaya, wameacha kwenda kanisani isipokuwa siku ya Krismasi na Pasaka au kwenye harusi na msiba.
Pia kutokana na mgawanyiko wa madhehebu kumekuwa na mkanganyiko kuhusu kazi ambazo zinaipasa kanisa la leo.
SALA NA IBADA
Mafundisho ya Yesu kuhusu sala hayatii maanani taratibu maalum, badala yake yeye alisisitiza msimamo wa ndani wa kumuendea Mungu kwa imani na unyofu kama vitoto vinavyohusiana na baba zao.
Ndivyo mwenyewe alivyosali katika roho mtakatifu aliyewaahidia wafuasi atawaongoza badala yake.
Kwa msingi huo, katika historia ya kanisa namna nyingi za kusali zimetokea kwa maisha ya kiroho ya Mkristo binafsi na kwa jumuiya nzima pamoja.
Kwa kawaida taratibu za kuendesha ibada zinaitwa Liturujia (kutoka kwa maneno ya Kigiriki yenye maana ya "kazi ya hadhara".
Wakatoliki, Waorthodoksi, Waorhodoski wa mashariki, Waanglikana, Wamethodisti, Walutheri na wengineo wanafuatilia desturi kama walivyozipokea.
Mtiririko wa ibada zao huandikwa na kujulikana kama Liturujia, madhehebu mengine, hasa yake ya Kipentekoste huwa na ibada ambazo hazijaandikwani kitabuni.
Kiongozi wa ibada wa siku hiyo huja na madondoo yake na mtiririko wa ibada huenda kama "roho" atakavyoongoza siku hiyo, kwa sababu hiyo husema kwamba hawafuati desturi au mapokeo.
Ukiangalia zaidi utaona kuwa ibada zao pia huwa na mtindo na mtiririko fulani, kama vile kuimba mapambio ya haraka haraka wakiwa wanapiga makofi, kucheza na kurukaruka.
Mapambio hayo hufuatiliwa na mengine ya taratibu wakiinua mikono kuabudu, inawezekana kusema hao nao wana utaratibu au Liturujia Yao ingawa haijaandikwa kwenye vitabu.
INAENDELEA
