Simba yaendeleza vipigo Sheikh Amri Abeid
TIMU ya Simba SC imeibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Fountain Gate katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara jioni ya leo Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Jijini Arusha.
Mabao ya Simba SC yamefungwa na kiungo Mzambia, Clatous Chotta Chama dakika ya 45’+7, winga Msenegal Libasse Gueye dakika ya 53 na kiungo mzawa, Shaaban Mgunda aliyejifunga dakika ya 71 wakati akijaribu kuokoa.
Kwa matokeo hayo, Simba SC inafikisha pointi 39, ingawa inabaki nafasi ya pili ikizidiwa pointi tano na mabingwa watetezi, Yanga SC baada ya timu zote kucheza mechi 18.
Kwa upande wao Fountain Gate baada ya kupoteza mchezo wa 10 leo kati ya michezo 18 iliyocheza hadi sasa, mingine minne ikitoaa sare na kushinda minne pia – inabaki na pointi zake 16 nafasi ya 14 katika ligi ya timu 16.
Ikumbukwe mwisho wa msimu timu mbili zitashuka Daraja na mbili zitakazomaliza nafasi ya 14 na 13 zitamenyana baina yao kwa mechi mbili za nyumbani na ugenini na mshindi wa jumla atasalia Ligi Kuu.
Timu itakayofungwa itakwenda kumenyana na timu kutoka Ligi ya Championship katika mechi nyingine mbili za mchujo nyumbani na ugenini na mshindi wa jumla ndiye atacheza Ligi Kuu msimu ujao.
