Pedro Goncalves awakomalia wachezaji wa Yanga kushinda kila mechi
Kocha Mkuu wa Yanga, Pedro Gonçalves, amesema wachezaji wake wanapaswa kujituma kikamilifu bila kujali wanakutana na timu gani, iwe Al Ahly SC au TMA, katika kuelekea mchezo wa Kombe la Shirikisho la CRDB.
Akizungumza na waandishi wa habari kuelekea mchezo huo wa kesho, Gonçalves amesema Yanga inaelekea kwenye mashindano yenye hadhi kubwa, hivyo wanahitaji kushinda ili kufuzu hatua inayofuata.
Amesema wachezaji wanapaswa kucheza kwa bidii na umakini, akibainisha kuwa kushindwa kuzingatia hilo kunaweza kuwaweka katika hali ngumu, kwani wapinzani wao hawana cha kupoteza.
“Tunajua tukipoteza kesho tutakuwa tumepoteza nafasi ya ubingwa, lakini tukitekeleza kila jambo ipasavyo tuna nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa tena,” amesema Gonçalves.
Aidha, amesema TMA wanafahamu kuwa mchezo huo ni jukwaa muhimu la kuonesha uwezo wao, hivyo Yanga haitawabeza wapinzani wao licha ya kwamba waliitoa timu ya Ligi Kuu.
Kwa upande wake, mchezaji wa Yanga, Allan Okello, amesema wapinzani wao hawana cha kupoteza, hivyo ni muhimu kwa Yanga kucheza kwa umakini na heshima.
Amesema kushindwa kwa Yanga kunaweza kuwa habari kubwa, hivyo wachezaji wanapaswa kubaki kwenye malengo na kutoidharau timu yoyote.
“Mpira unahitaji heshima kwa kila mpinzani. Nguvu tunayotumia dhidi ya timu za Ligi Kuu inapaswa kutumika pia ili kuonesha utofauti,” amesema Okello.

