MADUDU YA WAAMUZI WA TANZANIA, TFF ICHUKUE WA NJE
Na Prince Hoza Matua
KWANZA namshukuru mwenyezi Mungu kwa kunipa uzima ambao unanifanya leo niandike makala maalum ya MIKASI ambayo kila siku ya Alhamisi inawajia, lakini pia namshukuru kwa kuniwezesha kuuona mwaka wangu mpya.
Ikumbukwe Machi 31 majuzi ya wiki hii nimeadhimisha siku ya kuzaliwa (Happy Birthday) ambapo mimi na familia yangu tulikuwa na furaha ya kutimiza siku za kuzaliwa ya mpendwa wao (Prince Hoza).
Naenda kwenye mada kama ilivyo kawaida yangu kuwaletea mjadala ambao unawahusu wasomaji wangu kutoka pande mbalimbali ulimwenguni.
Mjadala wangu unahusu waamuzi, hasa wale wanaochezesha michuano ya Ligi Kuu bara, kombe la CRDB, Ngao ya Jamii, kombe la Mapinduzi na kombe la Muungano.
Lakini pia waamuzi wetu ni mahususi kwa kuchezesha mechi za kirafiki za timu zetu kubwa zinazoshiriki mashindano makubwa ya nchi na pia ligi ya Championship.
Nikielekea zaidi kwenye Ligi Kuu bara, ushindani wa ligi ni mkubwa na safari hii timu zote kubwa za Yanga SC, Simba SC, Azam FC na Singida Black Stars zinakutana na ushindani mkali.
Ila kitu kinachonipa wasiwasi ni kwamba waamuzi wanaopewa jukumu la kuchezesha mechi mbalimbali za ligi hiyo wanashindwa kusimamia vema Sheria 17 za FIFA.
Zipo baadhi ya mechi za Ligi Kuu bara maamuzi yake hayakuwa sahihi, tumeona hatua mbalimbali zikichukuliwa na Bodi ya Ligi kupitia kamati yake ya masaa 72 ambapo waamuzi wamekuwa wakitozwa faini na kufungiwa.
Wapo waamuzi wanaofungiwa miezi 6 mpaka miezi 12 na wengine wakishushwa daraja na kufutwa kabisa, suala la waamuzi limekuwa tatizo kubwa kiasi kwamba kero imezoeleka huku timu zikiumia.
Ushauri wangu kwa wasimamizi wa mpira wa hapa nchini, TFF kuanza hatua ya kutumia waamuzi wa nje ya nchi, msimu uliopita TFF iliamua kuchukua waamuzi kutoka nchini Misri kuchezesha mpambano wa watani wa jadi kati ya Simba SC na Yanga SC.
Mchezo huo ulifanyika katika uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam ambapo Yanga SC iliibuka na ushindi wa mabao 2-0, kila mtazamaji aliyeshuhudia mchezo huo aliridhishwa na maamuzi mazuri ya waamuzi wa mchezo huo.
Waamuzi wetu wa Tanzania bado hawajiamini wanapopewa filimbi ama vibendera Ili kuamua mchezo husika, sijui wanaogopa lawama za mashabiki hasa wa hizi timu kubwa zenye mashabiki wenye hisia kali.
Wapo baadhi ya waamuzi wa Tanzania ambao kidogo wamejipatia sifa kemkem lakini nao wanapopewa nafasi ya kuamua mechi za mahasimu ujikuta wanaingia mchecheto na kutoa maamuzi ambayo ni mshangao kwa wengine.
Waamuzi wetu wamejawa na hofu, nadhani tatizo lipo kwa timu kubwa ambazo zenyewe hazitaki kupoteza mchezo, mashabiki wa timu hizo hawataki kuona timu zao zikifungwa ama kutoka sare, lawama zote huwabebesha waamuzi na hapo ndipo huwafanya kuwa waoga.
Ni vema Rais Wallace Karia na kamati tendaji yake ya TFF ifikirie kwa kina kutumia waamuzi wa kutoka nje ya mipaka yake wenye beji ya CAF ambao wanasifa ya kuchezesha michuano mbalimbali ya Afrika.
.........................................
Kolamu ya MIKASI Inaletwa kwenu kwa hisani ya Angaxa House, wauzaji, wapangishaji nyumba, viwanja nk wanaopatikana jijini Dar es Salaam kwa simu namba 0652-626627.
ALAMSIKI
