Uongozi wa klabu ya Young Africans SC, chini ya Rais Eng. Hersi Said, umezidisha kasi ya kutekeleza ahadi ya ujenzi wa uwanja wa klabu hiyo baada ya kufanya kikao cha pili cha kimkakati na ofisi za TARURA pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo.
Kikao hicho kilichofanyika leo kimelenga kupokea na kujadili uwasilishwaji wa ramani ya awali pamoja na maelezo ya kina ya kitaalamu kuhusu mradi huo, hatua inayozidi kuwapa matumaini mashabiki wa "Wananchi" kuona klabu yao inamiliki miundombinu ya kisasa.
Katika kikao hicho, wadau na wataalamu wamejadili mambo muhimu yanayohusu utekelezaji wa mradi, ikiwa ni pamoja na ukaguzi wa eneo na taratibu za kisheria na kiufundi ili kuweka msingi imara kabla ya ujenzi kuanza rasmi.
Eng. Hersi amesisitiza kuwa dhumuni la klabu ni kuhakikisha mradi huu unatekelezwa kwa kiwango cha juu cha weledi, jambo ambalo litaifanya Yanga SC kuwa miongoni mwa klabu chache barani Afrika zinazomiliki viwanja vyenye sifa za kimataifa, hivyo kuimarisha zaidi chapa yao kibiashara na kimichezo.
