Gwiji wa soka nchini Senegal na Afrika, El Hadji Diouf, ametoa kauli ya kijasiri na yenye utata kuhusu hatima ya timu yake ya taifa kufuatia mchakato wa kisheria unaoendelea katika Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS).
Diouf amesisitiza kuwa ikiwa Senegal itafanikiwa kuibuka na ushindi kwenye kesi hiyo, basi wanapaswa kuongezewa nyota ya tatu kwenye jezi yao kama ishara ya ushindi uliopatikana ndani na nje ya uwanja.
Kwa mujibu wa maelezo, Diouf anaamini kuwa ushindi wa kisheria ni sehemu ya mafanikio ya mchezo, na hivyo unapaswa kutambuliwa rasmi kwenye utambulisho wa timu hiyo (Crest).
Kauli hii ya mshambuliaji huyo wa zamani wa Liverpool imezua mjadala mpana miongoni mwa mashabiki wa soka barani Afrika, huku wengi wakijiuliza juu ya uzito wa kesi hiyo kule CAS na namna ambavyo matokeo yake yanaweza kubadili historia ya soka la Senegal ambalo tayari lina mafanikio makubwa katika miaka ya hivi karibuni.
