ALIYEKUWA Mwenyekiti na Mwasisi wa Singida Black Stars, Yusuph Mwandami amefariki dunia jana baada ya gari alilokuwa wakisafiria kusombwa na maji katika Mto Mang’onyi, Singida.
Ajali hiyo imechukua pia na uhai wa mke wa Mwandami, Luluwa Suleimani na mtoto wao, Sabri Yusuph pamoja na dereva wao ambao wote walisombwa na maji katika Mto Mang’onyi.
Taarifa zinasema hadi jana kufikia Machi 27, 2026, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Singida lilikuwa limefanikiwa kuopoa miili ya Yusuph Mwandami na mke wake, Luluwa Suleiman pekee.
Ajali hiyo ilitokea wakati familia hiyo ikijaribu kuvuka mto huo uliokuwa na maji mengi na tukio hilo limeacha simanzi mkoani Singida kutokana na mchango wake katika uongozi na sekta ya madini.
Pamoja na Uenyekiti wa Singida Black Stars, Mwandami pia alikuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Singida na mmiliki wa mgodi wa dhahabu wilayani Ikungi.
Klabu ya Singida Black Stars imetoa pole kufuatia msiba huo mzito. “Tumepokea kwa masikitiko makubwa msiba huu mzito. Tupo pamoja na familia, ndugu, jamaa na wadau wote wa soka mkoani Singida katika kipindi hiki kigumu. Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi. Amina,” imesema taarifa ya Singida Black Stars.
Mungu awalaze pema peponi. Amin.
