Rais wa Heshima wa Simba SC na mfanyabiashara, Mohammed Dewji ameshuka kwa nafasi mbili katika chati ya mabilionea Afrika kwa mujibu wa ripoti ya jarida na mtandao wa Forbes ambayo imetoka Jumatatu, Machi 9, 2026.
Kwa sasa Dewji anashika nafasi ya 14 akiwa na utajiri ambao unatajwa kufikia kiasi cha Dola 2.1 bilioni (Sh5.4 trilioni) ukichangiwa na uwekezaji katika viwanda vya nguo, unga wa ngano na sembe, mafuta ya kupikia, sabuni, sukari, vinywaji na biashara ya katani.
Kabla ya orodha hiyo ya mabilionea ya kwanza kutolewa kwa mwaka 2026, Dewji alikuwa nafasi ya 12 katika orodha ya mwisho kwa mwaka 2025 iliyotoka Desemba 8, 2025 akiwa na utajiri uliokadiriwa kufikia Dola 2.2 bilioni (Sh5.7 trilioni).
Wakati Dewji akishuka kwa nafasi mbili, Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), Patrice Motsepe amependa kwa nafasi moja kutoka ile ya tisa aliyokuwepo Desemba mwaka jana hadi ya nane.
Utajiri wa Motsepe umepanda hadi kufikia kiasi cha Dola 4.3 bilioni (Sh11 trilioni) kutoka ule wa Dola 3.6 bilioni (Sh9 trilioni) aliokuwa nao Desemba, 2025.
Orodha hiyo ya mabilionea Afrika inaendelea kuongozwa na Aliko Dangote wa Nigeria ambaye utajiri wake umepanda hadi kiasi cha Dola 28.5 milioni (Sh74 trilioni).
