Kiungo wa kimataifa wa Nigeria na klabu ya Molde ya nchini Norway, Daniel Daga, ameingia kwenye msukosuko mkubwa wa kisheria baada ya kuhukumiwa kifungo cha miezi sita jela..
Hukumu hiyo imetolewa na Mahakama ya Wilaya ya Nordmøre na Romsdal nchini humo, kufuatia mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 19 kupatikana na hatia ya kuhusika katika kitendo cha kingono bila ridhaa.
Licha ya hukumu hiyo nzito, Daga pia ameamriwa kulipa faini ya Kroner 10,000 za Norway kwa ajili ya gharama za kesi.
Hata hivyo, mchezaji huyo kupitia mawakili wake amekata rufaa dhidi ya uamuzi huo, jambo linalomaanisha kuwa hukumu hiyo haitaanza kutumika mara moja mpaka pale mchakato wa rufaa utakapokamilika katika mfumo wa sheria wa Norway.
Kufuatia sakata hilo, klabu yake ya Molde tayari imemsimamisha mchezaji huyo kushiriki mazoezi na shughuli zote za timu tangu tuhuma hizo zilipoibuka miezi miwili iliyopita.
Uongozi wa klabu hiyo umethibitisha kuwa Daga ataendelea kubaki nje ya kikosi wakati taratibu za kisheria zikiendelea, jambo ambalo linaweka rehani mustakabali wa kipaji hicho kilichowahi kung'ara na timu ya taifa ya Nigeria ya vijana (U-20) katika Kombe la Dunia.
