Inaandikwa na Fikiri Salum
ILIPOISHIA
MTUME akamjibu "mimi sijui kusoma kwani sijapata kujifunza", akaja akamkamata, akambana akamwambia tena "soma", mtume akamjibu jawabu lile lile, hata mara ya tatu akamwambia "soma" iqra a bismi ra bbik.
Endelea.
Akamsomea sura ya 96 mpaka kati yake kisha mtume akaisoma kama alivyosomewa, hii ndiyo sura ya kwanza kushika katika kurani, ingawa haijawekwa mwanzo.
Mara yule mtu (malaika) akaondoka mwchoni pake asimwone, kaenda wapi, naye akarejea kwake hofu imemshika.
Alipofika nyumbani Khadija alidhani ana homa, akamfunika nguo gubigubi akakaa mbele yake akimsikiliza anavyoweweseka, homa ilipomwachia alimweleza Khadija yote yaliyomtokea, naye akamtuliza moyo wake, akamyakinishia ya kuwa hapana lolote baya litakalomzukia.
Mara bibi huyu akaondoka, akaenda kwa jamaa yake Waraga bin Naufat akampa habari yote iliyompata mumewe, naye akamwamrisha amwite na mtume akaenda akamweleza habari yake yote.
Bwana Waraga akamwambia "huyo ndiye Jibril, aliyemshukis Nabii Musa na Nabii Isa, basi jibashirie kuwa wewe ni mtume wa umma huu! Nami natamani kuwa hai nikuone unavyosimama kuwatengeneza jamaa zako, inshallah nitakuwa mkono wako wa kulia.
Wakarejea kwao hofu yote imemtoka baada ya kuazimia kuwa hatakwenda tena kule pangoni, palepale akaondoka akaenda pangoni mwake Ili aonane na makike tena, ingawa alikaa huko muda mrefu.
Siku Ile ya kupata utume inafikia mwezi Disemba 610, huyu Waraga hakuwa akiabudu dini ya sanamu bali alikuwa Mkristo, alipokuwa akisoma vitabu aliona kutatokea mtume mwingine, ndiyo maana alipohadithiwa habari Ile mara moja akaamini kuwa aliyemjia mtume ni Jibril.
MAISHA YAKE MAKKAH
Muhammad aliishi Makkah kwa miaka 53, arobaini (40) katika hiyo akiwa ni mtu wa kawaida kabla ya kupewa utume, na 13 akiwa ni mjumbe wa mwenyezi Mungu.
Maisha yake Makkah yalikuwa ya taabu utotoni mwake, kwani alizaliwa yatima kisha alipokuwa katika ujana wake alikuwa akifanya kazi ya kuchunga mbuzi na kondoo na watu wa Makkah kwa vijipesa kidogo mpaka alipofika umri wa miaka 25 akapata kazi ya kumfanyia biashara Khadija, bibi mtukufu wa Kikureshi ambaye baadaye alikuja kuwa mkewe na kuzaa naye aghlabu ya watoto wake.
MIAKA 13 YA UTUME MAKKAH
Katika miaka 13 aliyoishi hapo Makkah baada ya kupewa utume, Muhammad alipata kila aina ya mateso na masumbuko, juu ya nafsi yake na juu ya wafuasi wake, naye alisubiri na kustahimili kila aina ya taabu na shida kwa ajili ya mola wake, mpaka mwenyezi Mungu alipompa amri ya kuhama mji huo na kuelekea Madina.
Katika muda huo alipokuwa Makkah wengi wa jamaa zake na watu wengine wakubwa wa matabaka mbalimbali za jamii waliingia dini yake.
Mwaka 622 Wakureshi wakiona hasara katika mafungamano yao na Waarabu wengi wenye kuabudu miungu mingi kwa dukuduku zao zilimfanya Muhammad ahamie pamoja na sahibu wake Abubakar Assiddiq na wafuasi wake 70 hivi akaishi Yaithrib, mji ambao ulikaliwa na Waarabu na Wayahudi pamoja na ambao baadaye ukaitwa Madinat Al Nabi, yaani mji wa Nabii kifupi kifupi Madina.
Mwaka huo ukawa wa kwanza katika kalenda ya Kiislamu inayotumika tangu wakati wa Halifa Omar bin Khatab hadi leo.
KUHAMIA MADINA NA MWANZO WA UMMA
Mtume Muhammad baada ya kupewa amri ya kuudhuria Madina aliondoka na kuhama mji huo ambao ulimpokea na kumkubali na kumsaidia na kuntukuza na kumlinda na maadui.
Ingawa Wayahudi wa Madina walikataa kumsadiki kuwa nabii, kama wale wa Biblia, aliendelea kuhubiri huko na tangu mwaka wa kwanza alitunga hati ya Agano iliyokubaliwa na Wamadina wote ndiyo asili ya umma, jamii ya waumini.
INAENDELEA
