Inaandikwa na Fikiri Salum
MUHAMMAD kwa Kiarabu (mwenye kusifika) jina kamili ni Muhammad bin Abd Allah bin Abd Al-:Muttalib Al Hashim anaashiriwa katika dini ya Uislamu kuwa ni MTUME wa mwisho wa mwenyezi Mungu (Allah) kwa binadamu.
UTOTO WAKE
Muhammad alizaliwa yatima, kwani baba yake alifariki kabla yeye hajazaliwa, hakuishi sana na mama yake (Amina) kwa kuwa naye alifariki dunia, Muhammad akiwa na umri wa miaka sita.
Baadaye akachukuliwa na babu yake Abdul Muttalib na kuishi naye kwa muda wa miaka miwili, kisha babu yake naye alifariki.
Kazi ya kumlea Muhammad ilimwangukia ami yake Abu Talib ambaye ndiye aliyeishi naye mpaka ukubwa na kumuoza na kumpa himaya wakati alipoanza kazi ya kufikisha ujumbe wa mwenyezi Mungu kwa watu.
Kadiri ya hadithi za Kiislamu, ilipokuwa karibu atadhihiri mtume, mapadri wa kinasara na makuhani wa Kiyahudi waliokuwa wakikaa Bara Arabu walikuwa wakiwatayarisha majirani wao wa Kiarabu waliokuwa wakiabudu sanamu, wakiwaambia "karibu ataletwa mtume katika nchi yenu hii, abatilishe hii ibada yenu mbovu ya sanamu".
Walipoambiwa hivi wale Waarabu waliwauliza jina la mtume huyo, wakawajibu kuwa jina lake litakuwa Muhammad kwa hivyo kila mwenye kusadiki hayo alimwita mwanaye Muhammad.
Lakini hayakusikilizana majina haya ila kwa baadhi ya Waarabu waliokua wakikaa Shamu tu na Najran, (Yemen), ambako mapadri wengi walikaa, na vile vile katika Madina ambayo nusu ya wakazi wake walikuwa Wayahudi.
Hata lilipoanza kutangaa jina la mtume, waliokuwa wamekwisha kuitwa kwa jina hilo walikuwa wachache tu Bara Arabu nzima.
Inasemekana mtume aliinukia tangu utotoni kwake juu ya sifa zake nzuri na ukomavu wa akili ya kiutu uzima, hakupata kufanya vitendo vya utoto umri wake, wala kuazimia kuvifanya ila mara mbili tu ambazo mara zote hizo mwenyezi Mungu alimhofadhi navyo.
Kitendo chenyewe alichokiazimia kukifanya mara mbili zote hizo na mwenyezi Mungu akamfadhi nacho ni kutaka kukesha katika ngoma za Arusi.. ITAENDELEA JUMATATU IJAYO
