Na Prince Hoza Matua
TIMU ya Azam FC imefanikiwa kwenda Fainali ya Kombe la Mapinduzi baada ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Simba SC usiku wa jana Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.
Pongezi kwa mfungaji wa bao hilo pekee, beki wa kati Lameck Elias Lawi dakika ya 73 na sasa Azam FC itakutana na mshindi wa Nusu Fainali ya pili hii leo kati ya Yanga SC na Singida Black Stars.
Huo ni ushindi wa pili kwa Azam FC dhidi ya Simba SC katika mechi zilizochezwa karibuni, kwani Desemba mwaka jana Azam FC iliifunga Simba mabao 2-0 katika uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam mchezo wa Ligi Kuu bara inayodhaminiwa na benki ya NBC ambao ni wadhamini wa kombe la Mapinduzi.
Lakini pia ni ushindi wa pili mfululizo wa kocha Florent Ibenge raia wa DR Congo ambaye tangu alipopewa jukumu la kuinoa Azam FC akitokea Al Hilal Omduman ya Sudan, amekuwa mwiba mchungu kwa Simba.
Katika mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu bara dhidi ya Azam FC, Simba ilikuwa inanolewa na meneja mkuu Dimitar Pantev raia wa Burgalia, na baada ya mchezo huo uongozi wa Simba na meneja huyo waliamua kusitisha mkataba wao na jukumu hilo akaschiwa Seleman Matola ambaye ni kocha msaidizi.
Lakini kiukweli mwenendo wa Simba ndani ya misimu minne sasa sio mzuri, licha kwamba msimu uliopita klabu ilipata mafanikio makubwa ya kufanikiwa kucheza fainali ya kombe la Shirikisho Afrika, ila mimi nasema ukweli mwenendo wa Simba si mzuri.
Simba ilikuwa inanolewa na Fadlu David's raia wa Afrika Kusini ambaye aliifanya timu hiyo icheze fainali, lakini nilivyoitazama kiundani nikaona sio nzuri kiushindani.
Kombe la Shirikisho Afrika ni shindano dogo na linaloshirikisha timu ndogo tofauti na Ligi ya mabingwa barani Afrika, na ndio maana hata timu za madaraja ya chini zinapata nafasi ya kushiriki michuano hiyo.
Kundi ambalo walipangwa Simba lilikuwa dhaifu na ndio maana ilitoboa kiwepesi, lakini ilikutana na ushindani mkubwa kwenye ligi ya ndani pale ilipokutana na washindani wake wakuu Yanga na Azam ambapo Simba ilishindwa kuondoka na pointi ya ushindi na kujikuta ikiukosa ubingwa wa bara.
Tatizo kubwa la Simba tangu chini ya Fadlu ni kukosa wachezaji bora wanaoweza kuamua mechi kubwa, Simba imekuwa na tatizo na imekuwa ikikosa mtu wa kusimama kidete na kuishika timu pinzani kwenye mchezo ambao Simba inatakiwa kushinda.
Ushindani wa ndani, Simba inaonekana kuzidiwa pindi inapokutana na Yanga, Azam na hata Simba, malalamiko yao makubwa kwa mashabiki wake pindi ikishindwa kupata matokeo, wanayopeleka kwa kocha msaidizi Seleman Matola wakisema anawahujumu.
Lakini pia shutumu wanazipeleka kwa mwenyekiti wao wa klabu Murtaza Mangungu, kiukweli hao wote wanaowalalamikia mashabiki sio wahusika wanaosababisha timu isifanye vizuri.
Wapo baadhi ya wanachama wa klabu hiyo wamegeukia ushirikina na wakaenda kwa Masheikh kushitakiwa kufanya kwao vibaya na kusoma albadiri Ili kusudi kumdhuru anayetajwa kuwa na muharibifu kwa timu yao.
Lakini ukweli ni kwamba Simba inatakiwa kufanya usajili wa wachezaji wenye quality kubwa na ikiwezekana waizidi Yanga na kutawala soka la Tanzania, Simba inatakiwa irudi kwenye njia yake kuu, itwae ubingwa wa bara, kombe la CRDB na Ngao ya Jamii, lakini ioneshe ushindani ngazi ya kimataifa hasa Ligi ya mabingwa.
ALAMSIKI
