Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Ulimwenguni (FIFA),
Gianni Infantino, amelaani vikali matukio ya utovu wa nidhamu yaliyotokea katika mchezo wa fainali nchini Morocco, akisisitiza kuwa vitendo vya vurugu na uamuzi wa kuacha uwanja havikubaliki.
Katika taarifa yake aliyoituma kwa AFP, Infantino alisema:
"Tunalaani vikali tabia ya baadhi ya 'mashabiki' pamoja na baadhi ya wachezaji wa Senegal na wafanyakazi wa kiufundi.
Haikubaliki kuacha uwanja wa michezo kwa njia hii, na vile vile, vurugu haziwezi kuvumiliwa katika mchezo wetu, si sawa kabisa."
Rais huyo alitumia fursa hiyo kuipongeza Morocco kwa uandaaji mzuri, akitaja kuwa ni maandalizi tosha kwa taifa hilo kuelekea kuwa mwenyeji wa Kombe la Dunia la mwaka 2030.
Kwa upande mwingine, kocha wa Morocco, Walid Regragui, alielezea kusikitishwa kwake na taswira mbaya ambayo soka la Afrika limeionyesha mbele ya macho ya ulimwengu kutokana na fainali hiyo iliyotawaliwa na machafuko. Regragui alibainisha kuwa uharibifu huo wa sifa ni mkubwa na kuongeza: "
Taswira tuliyotoa kuhusu soka la Afrika ilikuwa ya aibu sana. Kulazimika kusimamisha mchezo kwa zaidi ya dakika 10 huku ulimwengu ukiutazama si jambo la kawaida sana."
Kauli yake inaakisi hofu ya wadau wengi wa soka barani humu juu ya jinsi matukio kama hayo yanavyoweza kurudisha nyuma juhudi za kukuza hadhi ya mchezo huu kimataifa.
Kufuatia sakata hilo, Tume ya Nidhamu ya CAF inatarajiwa kutoa adhabu kali na ya muda mrefu dhidi ya kocha wa Senegal, Pape Thiaw, kwa kuhusika na uamuzi wa kuiondoa timu uwanjani (kutoa timu).
Hatua hii inakuja wakati Rais wa CAF, Dr. Patrice Motsepe, akiwa na msimamo thabiti wa kuhakikisha nidhamu inatawala ili kulinda heshima ya bara hili, akisisitiza kuwa "Tunaendesha Afrika kwa ajili ya Waafrika."
