Nyota wa kimataifa wa Tanzania, Novatus Dismas Miroshi, amekuwa gumzo nchini Uturuki baada ya kufunga bao lake la kwanza msimu huu na kuisaidia klabu yake ya Göztepe kupata ushindi wa 3-1 dhidi ya Çaykur Rizespor katika mchezo wa Ligi Kuu ya Uturuki (Süper Lig) uliopigwa jana, Januari 19, 2026. Miroshi alifungua ukurasa wa mabao katika dakika ya 39 kwa shuti kali, huku mabao mengine ya Göztepe yakifungwa na Arda Kurtulan na Efkan Bekiroğlu. Ushindi huu umeifanya Göztepe kupanda hadi nafasi ya nne katika msimamo wa ligi ikiwa na alama 35, ikizitisha klabu kubwa kama Beşiktaş.
SHIRIKISHO la Soka Afrika (CAF) limetoa orodha ya viwango vya ubora wa klabu barani, Simba ikiendelea kuwa juu ya klabu nyingine za Tanzania, nafasi ya tano. Orodha hiyo imetoka leo kuelekea droo ya hatua za awali za michuano ya klabu Afrika ambayo kwa mara ya kwanza kihistoria itafanyika nchini katika studio za Azam Tv, Tabata Jijini Dar es Salaam. Yanga ambayo kama Simba itashiriki Ligi ya Mabingwa — yenyewe inashika nafasi ya 12, wakati timu nyingine katika orodha hiyo ni Namungo FC wanaoshika nafasi ya mwisho, ya 75 kwa pamoja na Salitas FC ya Burkina Faso, Ahli Benghazi ya Libya na NAPSA Stars ya Zambia. Kwa msimu ujao mbali na Simba na Yanga kushiriki Ligi ya Mabingwa, Azam FC na Singida Black Stars zitashiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.
