Na Prince Hoza Matua
NAWATAKIA kheri ya mwaka mpya wa 2026 na pia nawapa pole wale wote ambao walipoteza ndugu zao mwaka jana, lakini wengine wameuona mwaka mpya ila hawapo sawa kiafya, mwenyezi Mungu awape uzima na kurejea kwenye utimamu wa afya kusudi tulijenge vema taifa hili la Tanzania na dunia kwa ujumla.
Bila shaka Watanzania tumeingia mwaka mpya wa 2026 tukiwa na furaha tele kufuatia timu yetu ya taifa, Taifa Stars kufuzu hatua ya 16 bora ya AFCON inayofanyika nchini Morocco.
Shukrani kubwa ziwaendee wachezaji, benchi la ufundi la timu hiyo na viongozi wa Shirikisho la soka nchini, TFF kwa kufanikisha timu hiyo inaandika rekodi ya mara ya kwanza kufika hatua hiyo.
Lakini kubwa ni kwa kaimu kocha mkuu wa timu hiyo Miguel Angel Gamondi raia wa Argentina ambaye uwepo wapo umesaidia timu hiyo kufika hapo, nitakuwa mchoyo wa fadhila kama sitawapongeza makocha wengine waliofanya vizuri aliwemo Hemed Morocco ambaye alikuwa kocha mkuu wa timu hiyo.
Morocco akisaidiana na Juma Mgunda na Jamhuri Kihwelu Julio walisaidia timu hiyo kufuzu fainali za AFCON za mwaka 2025 zinazoendelea Morocco, hivyo ba wao huenda leo hii tusingezungumza chochote kuhusu Taifa Stars.
Miguel Gamondi alipewa jukumu la kuinoa Taifa Stars kama kaimu kocha akichukua mikoba ya Hemed Suleiman Morocco na moja kwa moja aliingiza timu kambini kujiandaa na AFCON.
Wengi tuliona kama miujiza kumpa Gamondi timu hiyo zikiwa zimesalia siku chache kabla ya kuanza kwa fainali zenyewe, kwani muda wa maandalizi haukutosha kabisa, pia Gamondi alikuwa na kibarua kingine cha kuinoa klabu ya Singida Black Stars akiwa kama kocha mkuu.
Ikumbukwe Singida Black Stars ipo katika michuano ya kombe la Shirikisho Afrika na ikiwa imetinga makundi hivyo itakuwa ngumu kwa kocha huyo kujigawa kwenye majukumu mawili.
Kwa kifupi wengi tulijua kwamba Stars inakwenda kupiga maktaimu au kushiriki kwa mara nyingine, hakuna hata Mtanzania mmoja aliyeipa nafasi ya kusonga mbele timu hiyo, lakini pia hofu ilitanda wakiamini kwamba Gamondi hawezi kufika mbali kutokana na kundi ambalo imepangwa Taifa Stars ni gumu.
Taifa Stars ilipangwa kundi C na timu ngumu za Nigeria, Tunisia na Uganda ambazo zote zimekuwa tishio kwa Tanzania, nafasi ya mwisho iliandaliwa Stars na hata aliyekuwa kocha msaidizi wa timu hiyo Jamhuri Kihwelu Julio alisikika akibeza kuachwa kwao na kumpa Gamondi.
Julio aliamini kwamba Gamondi kama ni kocha bora zaidi yao basi awafilishe nusu fainali jambo ambalo ni kumbeza ingawa lolote linaweza kutokea kwenye soka, baada ya kuiwezesha timu hiyo kutinga hatua ya 16 bora AFCON, TFF sasa wanatakiwa kumuandalia mkataba wa kudumu.
Gamondi anapaswa kupewa mkataba wa kudumu kwa sababu ya jukumu kubwa lililo mbele ambalo yeye pekee anaweza kututoa kimasomaso, mwaka 2027 Tanzania itakuwa mwenyeji mwenza wa michuano ya AFCON hivyo ni bora tuanze maandalizi mapema.
Ushiriki wa Tanzania katika fainali za AFCON za mwaka 2025 nchini Morocco zilikuwa nzuri na tumepiga hatua hivyo michuano ijayo tuweke historia zaidi ikiwezekana tufike robo fainali au fainali yenyewe.
Kwa Gamondi inawezekana, kwani ni miongoni ya makocha ambao wanajitambua, kitendo cha kuibana Nigeria na Tunisia vilitosha kabisa kudhihirisha kwamba Stars ya Gamondi imefanya makubwa.
Kila la kheri wapenzi na wasomaji wa ukurasa wangu wa Mambo Uwanjani Blog.
ALAMSIKI
